Ndugu Wanahabari,
Assalam Aleykum
Kama mnavyojua kwamba kumetokea tukio la kusikitisha la kuvunjwa kwa
Makaburi ya Masheikh Wetu, wapendwa wetu, wazazi wetu na viongozi wetu
wa Dini ya Kiisalam, Marehemu Sheikh Yahya Hussein Na Marehemu Sheikh
Kassim Bin Juma, Usiku wa kuamkia tarehe 10/4/2012 katika viwanja vya
Makaburi ya Tambaza Jirani na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Tukio hili, licha ya kusikitisha lakini limeziingizia fedheha
Familia hizi mbili za Masheikh Hawa na Kwa Waisalamu kwa Jumla. Kwa
Desturi na Sheria, Viwanja vya Makaburi ni mahala panapotakiwa
Kuheshimiwa kutokana na ukweli kwamba ni moja wapo ya sehemu za Ibada.
Hivyo basi kutokana na Tukio hilo ni dhahiri kwamba waliofanya
kitendo hicho wamekiuka mafundisho ya Dini ya Kiislamu na hivyo kutenda
kosa ambalo kiimani linaweza kusababisha Madhara Makubwa kwao wenyewe,
Jamii na Taifa kwa Jumla.
Kwa muktadha huo basi Familia ya Marhum Sheikh Yahya Hussein
imeumizwa kwa kiwango cha juu na tukio hilo hasa ikizingatiwa kuwa
Makaburi yaliyovunjwa ni la baba yetu na la aliyekuwa swahiba wake
mkubwa Mzee wetu Sheikh Kassim Bin Juma Pekee.
Hali hii inaonyesha kwamba kuna Chuki Binafsi, Udhalilishaji na
Njama za Kuhujumu familia yetu, Dini yetu na Waislamu kwa Jumla na
hivyo kitendo cha aina hii kinaweza kuliingiza Taifa katika migogoro
isiyo na Tija, kidini, Kisiasa, kiuchumi na kimaendeleo ya Jamii.
Hata hivyo Familia ya Marhum Sheikh Yahya Hussein imefarijika kuona
uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Dar es salaam Pamoja na Baraza Kuu La
Waisalamu wa Tanzania (BAKWATA) chini ya Mufti wa Tanzania Sheikh Mkuu
Issa Bin Shaaban Simba kulishughulikia kwa haraka suala hili katika
mawanda ya kuthamini, Mila, Desturi na Ibada za Makaburi.
Hatua hiyo inaonyesha ni jinsi gani Jamii nzima ilivyoguswa na kadhia
hiyo ambayo inahatarisha Usalama wa Nchi na raia kwa sababu Waumini na
wananchi wengine ambao ni wapenzi wa Viongozi hao wa Kidini wanaweza,
kutokana imani zao, kujichukulia sheria mikononi.
Hata hivyo uongozi wa Serikali Mkoa wa Dar es salaam na vyombo vyake
bado unatakiwa kuwa makini katika maagizo yake na utekelezaji wa kazi
zake hasa katika sehemu ambazo zinagusa hisia za watu kama Makaburi na
sehemu za Ibada ili kuepuka matukio yenye sura ya Hujuma kama tukio hilo
la makaburi ya Tambaza ambayo yanaweza kuleta mtafaruku ndani ya jamii
na kuvunjika Amani ya nchi.
Sisi kama Familia Ya marehemu Sheikh Yahya Hussein tunaiomba Serikali
na vyombo vyake iwasake na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale
wote waliohusika na hujuma hizi.
Pamoja na hayo familia inaona kwamba dawa ya kuepukana na matatizo
kama haya ni kujenga uzio katika eneo hilo ili kuhifadhi Makaburi hayo.
Kwa hiyo tunaiomba Manispaa ya Wilaya ya Ilala ijenge uzio katika eneo
la Makaburi ya Tambaza.
Kwa upande wetu, pamoja na nia nzuri ambayo Serikali imeonyesha ya
kutaka kuyajenga tena Makaburi hayo, lakini sisi kama Familia ya Sheikh
Yahya Hussein na Sheikh Kassim Bin Juma tumeamua kwamba tutajenga
Makaburi ya wazazi wetu kwa gharama zetu wenyewe.
Wabillahi Tawfiq
Alhajj Maalim Hassan Yahya Hussein
( Kwa niaba ya Familia )
Social Plugin