Baada ya miaka 13 ya kuwapo katika fani ya sanaa ya maigizo, hakuna shaka kwamba, Steven Jacob maarufu kama JB, kwa sasa ni miongoni mwa watu wenye majina makubwa mno katika fani hiyo nchini. Ni miongoni mwa nyota `Watano’ Bora zaidi wa kiume kwa upande wa fani hiyo, hivyo kumfanya kuwa katika hadhi ya juu, sawa na nyota wengine kama akina Steven Kanumba na Vincent Kigosi `Ray’ na wengine.
Ndiyo maana haishangazi kuona kwamba, hata leo hii ukiingia katika soko la filamu zilizo juu, huwezi kukosa kazi za nyota huyo.
Kwa sasa, JB, mtu mwenye umbo la miraba minne licha ya kucheza filamu ni mwandishi wa filamu na mtayarishaji, anatamba na ‘Illegal Sisters’, ‘Signature’, ‘Tanzanite’ na ‘Msamaha wa Rais’, Nakwenda kwa mwanagu, Dereva tax D.N.A na nyingine nyingi.
Katika mahojiano na tovuti hii hivi karibuni, JB anasema kwamba, ana kila sababu ya kujivunia mafanikio yake, ingawa hawezi kuvimba kichwa kwa umaarufu, huku akisisitiza alianza kuigiza kama mzaha na baadaye taratibu fani ikamkolea na kuigeuza sehemu ya maisha yake.
Anasema kwamba, alikuwa `anaburuzwa’ na rafiki yake, Single Mtambalike ‘Richie Richie’ ajiunge na kundi lao la wasanii wanne lililoitwa Four For You ambalo mbali ya Richie, wengine walikuwa Anna Costantine `Waridi’, Allen Raymond `Bishanga’ na Aisha.
“Kwa kuwa tulikuwa pamoja muda mrefu katika maskani pale Sinza Kijiweni, nilihisi kama nabughudhiwa, nikawa nakwenda mazoezini kila jioni, ingawa wakati mwingine nilikuwa nawakimbia,” anasema JB akisimulia alivyoingia kwenye maigizo na baadaye filamu mwaka 1997.
Mwaka mmoja baadaye, yaani mwaka 1998, akajiunga na kundi hilo rasmi ili kumfurahisha Richie na mwaka 1999 kundi hilo lilitoa mchezo, `Kuvuja kwa mitihani.’ Anasema katika zoezi la kuboresha kundi waliwaongeza wasanii, kama Suzane Lewis `Natasha’ na mwanawe Yvonne Cherie `Monalisa’.
Aliongezeka pia George Otieno `Tyson’ ambaye baadaye alimuoa Monalisa. Kutokana na kukua kwa kundi hilo, walilibatiza Nyota Enssemble. Baada ya kuvuma kwa mchezo wa kwanza, akaja kupata moyo kutokana na mchezo wa ‘Nyota’ ambao ulikuwa mrefu kuliko wote nchini.
Alizidi kuipenda sanaa hasa baada ya kupata hamasa kutoka kwa wasanii wa mchezo wa Tausi, kutoka Kenya Kibibi na Dama walipoigiza sehemu ya igizo hilo. Akajiuliza juu ya maswali mengi kwanini wenzao waweze wao washindwe , na ndipo akajikuta akiongeza juhudi ingawa kwa kiasi kidogo sana.
Sifa kwa wasanii zikaanza kupanda, na kila mmoja kujiona anaweza kufanya zaidi ya mwenzake, kulipelekea mwaka 2002 Nyota Enssemble likajigawa na kutokea kundi lingine lililojulikana kama Nyota Academia. Katika kundi la Nyota Academia walitoka Monalisa, Natasha, Tyson, kwa kuwa JB, sanaa aliifanya kwa kumfuata Richie Richie, ikambidi ahame kumfuata alipo.
Nyota Anssemble ITV, ikabakiwa na Bishanga, Aisha, Waridi, Seki na wasanii wengine wachanga . Walipata nafasi CTN, na huko waliweza kuongeza wasanii wengine kama Vicent Kigosi `Ray’, Ben Kinyaiya, Macha na wengine ambao kwa pamoja walifyatua igizo moja la ‘Suzi’ na baada ya hapo walifanya igizo la mwisho na kundi likavunjika.
Baada ya kutamba katika maigizo, ndipo mwaka 2003 akageukia filamu, akiicheza kwa mara ya kwanza katika filamu ya `Masaa 24’. Kuanzia hapo aliunganisha filamu moja hadi nyingine, huku akijizolea umaarufu kila kukicha.
Na haikushangaza kuona akichaguliwa kuwa Mwigizaji Bora wa Kiume nchini katika tuzo za Vinara mwaka 2008. Kutokana na kuiva katika filamu, akaona sasa inatosha na hivyo kufikia kuanzisha kampuni yake.
Ndoto yake ilitimia mwaka 2005 baada ya kuanzisha kampuni aliyoiita Jerusalem. Hata hivyo, ilikuwa `mbinde’ kuanzisha Jerusalem, kwani hakuwa na fedha, hadi alipobebwa na Mohammed Mpakanjia `Kitendawili’ ambaye kwa sasa ni marehemu aliyempatia Sh milioni 1.5, huku Fujo naye akitoa kiasi kama hicho na hivyo kuanzisha rasmi kampuni.
Filamu ya kwanza ikawa `Kanisa la Leo’ mwaka huo huo wa 2005. Hata hivyo, Fujo alijitoa, hivyo kumlazimu JB kumtafuta mbia mwingine na kufanikiwa kumnasa swahiba wake, Richie Richie. Walitengeneza filamu za ‘Agano la Urithi’, `Stranger’, `Swahiba’ na `Kwa Heshima ya Penzi’. Baada ya filamu hizo, Richie naye akaachia ngazi na kuanzisha kampuni yake, Bulls Entertainment.
JB hakutetereka, bali aliimarisha zaidi kazi yake na kufyatua filamu nyingi zikiwamo Regina, My Fiance, Born Again, 14 Days, Signature na hivi karibuni anatarajia kuizindua filamu ya Zawadi ya Birthday aliyomshirikisha Richie.
Lakini nje ya filamu, JB ni Mwinjilisti na mfanyabiashara `mchakarikaji’ kweli kweli. Na hakuanza jana au leo, bali siku nyingi wakati huo akichukua mahindi mikoani na kuyauza Dar es Salaam. Biashara yake ilikua na kufikia hatua ya kumiliki kampuni ya usagishaji wa nafaka, akiagiza mahindi na kuuza unga kwa kutumia nembo ya `Sembe Mama’.
Kama si uzembe wake, hakika JB leo hii asingevuma kama msanii mahiri wa maigizo, bali kama mfanyabiashara mashuhuri kutokana na biashara zake kumwendea vyema tangu alipozianzisha mwaka 1996. Ni uzembe gani alioufanya JB? Mwenyewe hafichi, anasema kamari ndiyo iliyozamisha mtaji wangu na kumrudisha chini kabisa.
Katika hilo, mpaka leo anajutia uamuzi wake wa kuukumbatia mchezo huo, ambao anasema kwa siku ulikuwa `unamla’ kati ya sh laki mbili na wakati mwingine kufikia hata sh milioni mbili.
“Kamari imenifilisi sana na kunirudisha nyuma kimaisha.Kwa siku nilikuwa nacheza hata katika baa 15 hadi 20 bila kujua kuwa nilikuwa najiumiza mwenyewe. “Kutokana na uchezaji mkubwa wa kamari niliitwa jina la Binkololo, sababu ya yale makamari yalikuwa yakilia hivyo endapo mtu ukishinda. Marehemu Mpakanjia alinisihi niachane na kamari, lakini haikuwezekana hadi siku moja nilipoliwa fedha nyingi.”
Anakumbuka kwamba, siku hiyo alijiinamia, akatokea mzee asiyemjua na kumwambia, “Bora kamari ingekuwa inakula fedha zako, lakini inakuongezea nuksi katika maisha yako.” Maneno hayo yalimuingia vizuri na kuanzia hapo aliamua kuipa kisogo kamari.
Mbali ya kamari, sababu nyingine iliyomfilisi ni baadhi ya wateja wake wa mahindi kushindwa kulipa madeni, huku baadhi yao wakikimbia na fedha zake. Lakini baada ya misukosuko ya kibiashara, na kupata ujasiri akiwa katika ulimwengu wa maigizo na filamu, anasema sasa ana mengi ya kujivunia hasa Kampuni yake ya Jerusalem.
Anasema mbali ya mafanikio ya kazi za kisanii na kiuchumi, pia anajivunia kampuni yake kuwaibua wakali wa filamu kama Rose Ndauka, Elizabeth Kiyumba ’Nikita’, Steve wa Maisha Plus, Brigit mtangazaji wa EA TV, Lady Anifa na wengine.
Anasema Kampuni ya Jerusalem imemwezesha kufungua maduka jijini Dar es Salaam na kwamba sasa anajipanga kuifufua tena kampuni yake ya kusaga nafaka. “Na zaidi ya yote ni umaarufu na shughuli zangu zinaniwezesha kukidhi mahitaji yake yote ya msingi,” anasema JB ambaye anasema kwa sasa yeye ni mhubiri wa masuala ya dini na kwamba hata filamu zake zimeegemea katika upande wa dini, hasa ya Kikristo.
Akifafanua kuhusu `ulokole’ wake, anasema wakati wa kuigiza haimzuii kuingia mahali panapokwenda kinyume na imani za dini yake kwa sababu dhamira inakuwa kupata mazingira halisi ya sehemu anayoigiza.
Anakiri kwamba, hali hiyo si kwamba inawashangaza watu wa nje ya fani na familia yake, bali hata mkewe akidai haamini kama anaweza kushinda baa, klabu na sehemu nyingine bila ya kwenda kinyume cha imani yake.
“Wakati mwingine mke wangu anakosa, lakini kama ni mazingira fulani basi nafanya hivyo ili kuiga uhalisia wa filamu ninayoicheza,” anasema anayewahusudu kisanii Single Mtambalike kwa hapa Tanzania na Amitabh Bachan, gwiji wa filamu wa India tangu miaka ya 1970 ambaye katikati ya miaka ya 1980 alikuwa Mbunge nchini mwake.
Anamhusudu pia mwanamuziki na mwigizaji wa Marekani, Jeniffer Lopez `J.Lo’. Kwa upande wa filamu zake, anakiri Regina ndiyo anayoihusudu mno. “Niseme tu kwamba, ili kuiimarisha zaidi kampuni yangu, mwaka huu utakuwa wa mwisho kucheza filamu zitakazoandaliwa nje ya kampuni yangu kwa sababu naamini nina uwezo wa kufanya mambo makubwa nikiwa na Jerusalem,” anasema JB ambaye pia ni mkali katika mchezo wa soka akiwa sentahafu.
Makali yake aliyaonesha akiwa kambi ya JKT Mgambo mkoani Tanga alikokutana na Ramadhani Nassib, Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Mtaani, aliichezea timu Mutukuru ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam akiwa na makipa maarufu waliowahi kuzichezea Simba, Yanga na Taifa Stars, Joseph Fungo na Joseph Katuba ambaye kwa sasa ni marehemu.
Kwa upande wa elimu, alisoma Shule ya Msingi Forodhani alikohitimu mwaka 1984 na baadaye kujiunga na Sekondari ya Popatlal ya Tanga hadi mwaka 1988 na baadaye kidato cha tano na sita alikozamia katika masomo ya Uchumi na Biashara.
Kutoka hapo akaangukia JKT kwa mwaka mmoja. Huyo ndiye Jacob Steven ambaye hajabahatika kupata mtoto, kwani ndoa yake ndiyo kwanza ina mwaka mmoja.