TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
TAREHE
07.04.2014
CCM
MKOA WA SHINYANGA YA LAANI KAULI YA
MBUNGE
WA JIMBO LA KAHAMA JAMES LEMBELI
KUWA
“CCM SIYO MAMA YANGU”
Chama cha Mapinduzi
Mkoa wa Shinyanga KIMELAANI vikali kauli ya Mbunge James Lembeli Mbunge wa Jimbo
la Kahama aliyoitoa kwenye vyombo ya habari hivi karibuni iliyosema “CCM SIYO
MAMA YANGU”.
Kwa hiyo Chama cha
Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga na wana CCM wote kwa ujumla wamestushwa na kauli ya
Mbunge Lembeli anayetokana na CCM kwani kauli hii hatukutegemea sote kama ingeweza kutolewa na Mwanachama ambaye tena ni
Kiongozi ndani ya Chama.
Tunaomba ieleweke na
tunautaarifu Umma na wana CCM wote kuwa CCM haina tatizo kabisa na msimamo wa
Mbunge James Lembeli kuhusu msimamo wake wa serikali moja, mbili, tatu au nne
na hata serikali ya Tanganyika
kwani huo ni uhuru wake binafsi. Tatizo
letu kubwa kwake ni kauli aliyoitoa kuwa “CCM SIYO MAMA YANGU” kwani kauli hiyo
ameitoa sio mahali pake na haihusiki na utashi wake binafsi katika msimamo
alionao katika BUNGE LA KATIBA. Kauli
hii inaukakasi na ni sawa na kukinajisi Chama.
Lakini jambo la
ajabu na la kushangaza ni kuhusu kulitumia jina la Baba wa Taifa Mwl. J. K.
Nyerere vibaya, amekuwa akijifananisha na kauli ya Baba wa Taifa tungependa
atambue kuwa Lembeli hana hadhi na sifa ya kujifananisha na Baba wa Taifa;
kwani kujifafanisha kwake na Baba wa Taifa huko ni matumizi mabaya ya
kujitwisha sifa asizostahiki kwani Baba wa Taifa Mwl. J. K. Nyerere alikuwa na
karama, hekima na busara kubwa za pekee na aliheshimika Dunia kote pia alikuwa
anatoa kauli zake kutokana na mazingira yaliyokuwepo wakati huo.
Kwani Baba wa Taifa
kila jambo lililokuwa linahusu swala la Chama na Mstakabali wa Taifa alitumia
vikao kulizungumza sio anavyofanya Lembeli kuropoka ovyo, kutumia ubabe na
kukosa staha kwa Chama.
Tabia ya Mbunge
Lembeli ya kukidhihaki Chama imekuwa ikijitokeza mara kwa mara, lakini
tunapenda atambue na kumkumbusha kuwa Lembeli hapo alipofika na jeuri yote na
umaarufu alionao unatokana na CCM, kabla ya mwaka 2005 hakuna Mtanzania
aliyemfahamu popote nchini.
Lakini baada ya
kupewa ridhaa na CCM na hatimaye kuchaguliwa Ubunge ndipo akajenga umaarufu
uliotokana na CCM. Lakini jingine
tunapenda kumkumbusha kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 Lembeli alikuwa na
wakati mgumu sana ndani ya Chama na nje ya Chama lakini Chama na Wanachama
wakampigania kwa hali ya juu sana na kwa mazingira magumu na hatimaye ushindi
ukapatikana.
Leo shukrani anazotoa
kwa Chama ni kukiambia CCM SIO MAMA YAKE.
Basi na kama Lembeli
anaona CCM SIO MAMA YAKE ni vyema akatueleza MAMA YAKE NI NANI – KISIASA na kama ana MAMA MWINGINE KISIASA ni VYEMA AKAMFUATA HUYO
MAMA HUKO ALIKO anayeona atamfaa kumpa umaarufu zaidi ya CCM.
Mwisho CCM Mkoa wa
Shinyanga hakitakuwa tayari na hakitawavumilia wanachama na viongozi wake wenye
tabia kama ya Lembeli ya kuendelea
kukidhalilisha Chama hadharani.
Lakini pia Chama
kitaendelea kuheshimu Demokrasia ndani ya Chama na Uhuru wa mawazo unaofuata
maadili, miiko na taratibu za Chama ndani ya vikao.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Taarifa hii
imeandaliwa na Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga na imesomwa na:-
Ndugu
Emmanuel S. Mlimandago
Katibu
wa Siasa na Uenezi wa CCM
Mkoa
wa Shinyanga
05.04.2014