MWANAMUME mwenye umri wa makamo, Jumatatu
alisukumwa jela kwa miaka 15, kwa kumwambukiza mwanamke Ukimwi maksudi
wakifanya mapenzi.
Hakimu Mkazi
wa Iten, Bi Rose Ndombi, alimpa Gilbert Kiptoo Barbos adhabu hiyo baada
ya kumpata na hatia ya kufanya mapenzi na mwanamke huyo akijua kwamba
alikuwa na ukimwi.
Barbos
alipatikana na hatia ya kufanya mapenzi na mwanamke huyo mnamo Septemba
2, 2013, katika lojingi moja mjini Iten Kenya, akijua wazi kwamba alikuwa na
virusi vya ukimwi.
Mahakama
iliambiwa kwamba alifanya makosa hayo maksudi kwa kukosa kutumia kinga
wakati wa kitendo hicho akijua kwamba hatua hiyo, ingemfanya mwanamke
huyo aambukizwe ukimwi.
Mbali na kosa
hilo, Barbos alikabiliwa na mashtaka mengine mawili ya ubakaji na
wizi. Mahakama iliambiwa kwamba aliiba simu aina ya Techno ya mwanamke
huyo yenye thamani ya Sh3000 na Sh1000 pesa taslimu.
Mwendesha
mashtaka, Bw Tom Chitira aliambia mahakama kwamba Barbos, na mshukiwa
mwingine ambaye hakuwa mahakamani, walimwambia mlalamishi kwamba
wangemsaidia kupata kazi mjini Iten. Walipofika mjini Iten, Barbos
alimpeleka mwanamke huyo katika lojing’i ambako wangelala kabla ya
kumpeleka kwa mtu ambaye alidai angemwajiri.
Mlalamishi aliambia mahakama kwamba Barbos alimhandaa kwamba wangelala vyumba tofauti.
“Nafikiri
alinilewesha kabla ya kunipeleka katika lojing’i kwa sababu nakumbuka
nikikataa pendekezo lake la kulala chumba kimoja na mtu mgeni kwangu
kabla ya kujipata katika chumba alichokuwa siku iliyofuata,” mwanamke
huyo aliambia mahakama. Alisema alipiga ripoti katika kituo cha polisi
cha Iten na mshtakiwa akasakwa na kukamatwa.
Maafisa wa
polisi walimshauri mwanamke huyo aende kupimwa baada ya kupata dawa za
kuzima makali ya ukimwi (ARVs) walipomkamata Barbos.
Ripoti ya
daktari iliyowasilishwa mahakamani ilionyesha kwamba baada ya kupimwa,
iligunduliwa mlalamishi alikuwa ameambukizwa virusi vya ukimwi.
Ubakaji
Hata hivyo,
Bi Ndombi hakumpata Barbos na hatia ya ubakaji akisema upande wa
mashtaka haukuthibitisha shtaka hilo kulingana na viwango
vinavyohitajika kisheria, lakini akampata na hatia ya kuambukiza
mwanamke huyo ukimwi na kumuibia.
Akimhukumu,
Bi Ndombi alisema Barbos atafungwa jela miaka 15 ili kuwa funzo kwa
wengine wanaofanya makosa kama hayo. Alisema kwamba sheria iko wazi kwa
wanaoambukiza wengine ukimwi maksudi.
Alimhukumu
mshtakiwa kufungwa jela miezi sita kwa kosa la wizi na akaagiza kila
hukumu itekelezwe baada ya nyingine. Alimpatia mshtakiwa siku 14 za
kukata rufaa asiporidhika na hukumu hiyo.
Social Plugin