Viungo vingine ambavyo wauaji walitoweka navyo ni pua, kidevu, kidole gumba cha mguu wa kulia na nyama za mkono wa kushoto.
Mauaji hayo ya kikatili yamezua hofu kubwa kutokana na kuwapo mazingira yanayokanganya, baadhi yakihusishwa na imani za kishirikina na mengine kisasi.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wanakijiji wamekuja juu wakitaka uchunguzi wa kina ufanyike, ikiwamo baadhi ya viongozi wa kijiji hicho kuhojiwa.
Wanakijiji hao wanataka uchunguzi huo ufanyike kwa madai kwamba, kabla marehemu kufikwa na umauti, kulikuwa na mgogoro, ambao unafahamika.
Habari zilizopatikana kutokana katika kijiji hicho juzi na jana zinadai kuwa marehemu aliondoka nyumbani saa 3.00 usiku, Aprili 22, mwaka huu, akidai kwenda kwa mmoja wa jamaa.
Hata hivyo, habari hizo zinasema baada ya kuondoka, marehemu hakurejea hadi mwili wake ulipopatikana Aprili 25 mwaka huu, umbali wa kilometa mbili kutoka nyumbani kwake akiwa ameuawa na kunyofolewa baadhi ya viungo vya mwili wake.
Mmoja wa watoto wa marehemu, Jesca John, ndiye alielezea mazingira ya mama yake kuondoka nyumbani na kisha kutorejea hadi alipopatikana akiwa ameuawa.
Inadaiwa kuwa wakati huo mume wa marehemu alikuwa kwenye mji wake wa pili katika Kijiji cha Lumasa na kwamba, kumekuwapo na tetesi za kuwapo mtafaruku ndani ya ndoa yao.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, John Temu, alithibitisha kufanyika kwa mauaji hayo na kwamba, tayari mwanakijiji mmoja alikuwa anashikiliwa kutokana na tukio hilo. “Ni kweli mwandishi.
Baada ya kufuatilia kwa OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) wangu wa Chato imethibitika tukio hilo lipo na tayari mtu mmoja anashikiliwa kuhusiana na tukio hilo,” alisema Kamanda Temu.
Aliongeza: “Hata hivyo, tunajaribu kuingia kwa undani kutambua chanzo chake iwapo ni imani za kishirikina au mhalifu anaweza kutumia tu mwanya huo kupoteza ukweli kumbe hayatokani na imani za kishirikina.”
Kumewapo na taarifa za kukanganya katika kijiji hicho, ambazo baadhi zinadai kuwa mwaka jana kabla ya marehemu kufikwa na mauti, kuna matukio ambayo yaliashiria hali ya hatari kwake, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa kuweka mambo sawa.
Inadaiwa kuwa mwaka jana marehemu alikuwa kati ya wanawake watano waliofukuzwa katika kijiji hicho hadharani na viongozi wa kijiji kwenye mkutano ulioongozwa na viongozi wa ulinzi wa jadi sungusungu wa kijiji hicho.
Kwa mujibu wa habari hizo, wanawake hao walifukuzwa katika mkutano huo baada ya kutuhumiwa kuwa ni wachawi.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa tuhuma hizo zilipandikizwa na kuunga mkono na baadhi ya viongozi kutokana na chuki binafsi.
Uchunguzi wa kina uliofanyika katika kijiji hicho, umebaini kuwa marehemu na wanawake wengine waliotambuliwa kwa majina ya Bertha Musa, Bhati William, Ndebile Nyanda na Sweka Zacharia, walifukuzwa katika kijiji hicho.
Hata hivyo, baada ya malalamiko hayo kuifikia ofisi ya mkuu wa wilaya ya Chato na polisi, baadhi ya viongozi walikamatwa na kuamriwa kuwaruhusu wanawake hao, akiwamo marehemu kurejea katika kijiji hicho.
Hata hivyo, habari hizo zinasema kuwa hadi kufikia juzi, mmoja wanawake hao, Bahati William alikuwa hajarejea kijijni hapo kutokana na kile kinachodaiwa ni vitisho kutoka kwa baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kushirikiana na wanaotuhumiwa kuwafukuza kijijini hapo.
Hali hiyo inadaiwa kuibua mkanganyiko mkubwa juu ya kifo hicho.
Awali, Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Pastory Bugolo, katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi juzi kwa njia ya simu, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo.
Pia alithibitisha kuwa marehemu alikuwa miongoni mwa wanawake waliokuwa wamefukuzwa kijijini hapo wakituhumiwa kuwa ni wachawi.
Katika tukio jingine, wanakijiji wengine wanane wakazi wa kijiji cha Mwendakulima, Kata ya Buetengo-Lumasa, wilayani humo, wakiwamo wanawake, mwaka jana walifukuzwa kijijini hapo na baadhi ya viongozi wa kijiji hadharani wakituhumiwa kuwa ni wachawi.
Hatua hivyo inadaiwa kuyaweka hatarini maisha ya watuhumiwa na baadhi yao wanadai kuendelea kupewa vitisho na kwamba imekuwa vigumu kusikilizwa malalamiko yao kutokana na baadhi ya viongozi kuhusika.
Via>> Nipashe
Social Plugin