KUHUSU UGONJWA HATARI ULIOIBUKA JIJINI DAR ES SALAAM,WAUA MMOJA,WAATHIRI 10

Mbu anayeaminika kueneza homa ya dengue.
Ugonjwa wa homa ya dengue ulioibuka jijini Dar es Salaam kuanzia mwishoni mwa Januari, mwaka huu umeathiri watu 10 na mmoja amefariki dunia.


Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Donan Mmbando alisema hayo hivi karibuni alipozungumza na mwandishi na kusema baada ya kupungua kwa ugonjwa wa malaria,  umeibuka ugonjwa huo.


Alisema tangu uthibitishwe kuwepo nchini Januari mwaka huu, hadi  sasa idadi ya watu  ambao wamethibishwa kuugua ugonjwa huo ni 70. 

Kati ya hao,  58 ni kutoka Wilaya ya Kinondoni, saba  ni wa Temeke na  watano kutoka Ilala.

Kwa mujibu wa Dk Mmbando, katika  wiki mbili zilizopita,  idadi  ya wagonjwa imeongezeka mara mbili kuliko siku za nyuma. Alisema kifo kilichotokana na ugonjwa huo, kilitokea katika Hospitali ya Mwananyamala.

Alisema ugonjwa wa malaria umepungua kutoka asilimia 80 hadi chini ya 10 kutokana na kuwa juhudi zilielekezwa zaidi katika kudhibiti ugonjwa wa malaria pekee bila kujali wanaoambukiza magonjwa mengine.

“Mpango wa serikali sasa ni kudhibiti mbu wote wanaouma mchana na usiku bila kujali wanaambukiza magonjwa gani ili kuweza kupambana na homa hii inayoibuka kwa kasi,” alisema. 

Dk Mmbando alisema sasa wanaandaa taarifa muhimu na mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo na kutoa taarifa kwa wananchi.

Katika taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,  Dk Seif Suleiman Rashidi ilisema  ugonjwa huo si mpya nchini, kwani uligundulika kwa mara ya kwanza mnamo Juni  2010 mkoani Dar es Salaam, ambapo idadi ya watu waliothibitika kuwa na ugonjwa ilikuwa 40.

Alisema  pia kati ya Mei na Julai 2013, wagonjwa 172 walithibitishwa kuwa na ugonjwa huu na hakuna aliyepoteza maisha.

Waziri alishauri jamii  kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huo, isipokuwa waende kwenye vituo vya tiba wanapoona dalili. 

Alishauri wahakikishe mazalio yote ya mbu yanaangamizwa na pia kuzuia kuumwa na mbu. 

Alisema hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini. Alisema wizara itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali, kufuatilia na kudhibiti ugonjwa huu.
via>>habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم