Askofu Mkuu Kanisa la Anglikana
Tanzania, Dk Jacob Chimeledya ameonya tabia ya makasisi kutoa fedha ili
kununua Uaskofu kwani hiyo ni aibu.
Alisema hayo jana mjini Dodoma wakati
wa ibada ya maziko ya aliyekuwa Askofu wa Dayosisi ya Central
Tanganyika, Godfrey Mhogolo yaliyofanyika kwenye viwanja vya kanisa
hilo.
Alisema sasa kumekuwa na tabia ya kutafuta uaskofu wa kununua na watu wamekuwa wakitoa fedha ili wapate cheo hicho.
"Wakati mwingine watu wanatafuta na
kununua uaskofu ni kitu cha aibu, kwani kasisi anatafuta kwa gharama
yoyote ili awe askofu," alisema.
Alisema sasa wakati wa kujaza nafasi
hiyo utafika ili kanisa lisonge mbele na mchakato wa uchaguzi
utakapoanza wataomba ili apatikane kiongozi aliyeitwa na Mungu.
"Sisi tunasikia tayari mmeshaanza
kampeni kama zile wanavyogombea katika siasa, lakini ndani ya kanisa
hatunadi sera ni kuomba uongozi wa roho mtakatifu ili apatikane mtu wa
kujaza nafasi hiyo," alisema.
Kauli ya Askofu mstaafu Kwa upande wake,
Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa hilo, Donald Mtetemela pia aliwataka
wachungaji kuacha vita ya madaraka kutokana na kanisa kuingiliwa na
tabia za watu wenye tamaa za kutaka vyeo.
Alisema baadhi ya watu wenye kupenda
vyeo hatari wameanza kufikiri ni nani atashika nafasi hiyo alisema sasa
chuki na mioyo ya kuchafuana itainuka jambo ambalo si la kumpendeza
Mungu.
Aliwataka viongozi hao kulihurumia kanisa kwani vyeo ni vingi, lakini kuna mtu moja tu ambaye kanisa linamhitaji.
"Tuinue watumishi ambao watasimamia
kanisa lao vizuri, mtafuteni mchungaji ambaye ataendeleza kwa uaminifu
kanisa la Mungu," alisema .
Mtetemela alisema Askofu Mhogole alikuwa ni
mtu wa kuthubutu, kwani aliweza kuwekea mikono wanawake wawe wachungaji
pia alikuwa mtu wa kujadiliana sana na kanisa limempoteza kiongozi
mwenye mapenzi mema na watu.
Alisema wakati mwingine kanisa limepata
viongozi wanaoharibu kazi za Mungu na kutaka waumini waombe ili Mungu
aipatie dayosisi hiyo kiongozi mwingine mwaminifu.
"Wachungaji watulie, Bwana anawaona.
Tuache vita ya madaraka ndani ya kanisa," alisema na kuongeza kuwa,
Askofu Mhogole alianza kazi kama mhudumu wa ofisi, alifanya usafi,
kupika chai alipokea simu na kupeleka barua posta.
"Mahali popote Mungu anapokuweka ana sababu zake Mungu anapotaka kukuandaa wewe anakuweka kwenye kazi anayoona inafaa," alisema.
Alisema ni muhimu kwa watu kutumia fursa
wanazopata katika kazi kwa kuinua wengine na si kupata cheo na kutazama
namna ya kukomoa watu wengine.
Waziri Mkuu Pinda Kwa upande wake Waziri
Mkuu Mizengo Pinda alisema, Askofu Mhogolo alikuwa ni kiongozi makini
kwani aliweza kusimamia parishi 265 zenye makasisi zaidi ya 300 huku
waumini wa dayosisi ya kati wakiwa zaidi ya 600,000.
Alisema kazi nyingi alifanya kwenye
sekta ya afya, eli
mu na aliitumikia jamii na hata kukea na kusomesha
yatima jambo ambalo atazidi kukumbukwa.
"Uovu kila mmoja ana wa kwake,
lakini wema si kila mmoja anao, lakini changamoto kubwa ni kwa yule
atakayevaa viatu vyake kufanya mema au zaidi ya yale aliyokuwa
ameyafanya," alisema.
Maneno ya Malecela Kwa upande wake
Waziri Mkuu mstaafu John Malecela alisema atamkumbuka Askofu Mhogolo kwa
mema mengi ikiwemo tukio la kumfungisha ndoa na Anne Kilango miaka 11
iliyopita.
Alisema askofu huyo alikuwa ni mpenda
maendeleo na wakati akianza kazi kanisa lilikuwa likitegemea sana
wafadhili, lakini akasaidia sana kanisa kujitegemea.
Alisema sasa kanisa lina mali zenye
thamani ya Sh bilioni nane. Malecela alisema aliwahi kumsihi askofu huyo
ili hospitali ya Mvumi inayomilikiwa na kanisa hilo iwe hospitali ya
Teule ya Wilaya ya Chamwino alikubali na jambo hilo likafanyika.
"Alikuwa ni mtu aliyejali na msikivu
hatutamsahau daima," alisema Mchungaji Noah Masima alisema alilelewa na
kukua pamoja na marehemu askofu Mhogolo ambaye alipofikisha miaka 16
wazazi wake wote walifariki.
"Tulikuwa marafiki wa rika moja tulienda
shule pamoja darasa moja, michezo ya watoto pamoja tulitumia ulimbapo
kutafuta ndege porini, tukapigana mieleka baadaye nikachaguliwa kwenda
Mvumi Middle School yeye akaenda shuleni Chilonwa," alisema.
Alisema alipofikisha miaka 16, Mhogolo
alifiwa na wazazi wake wawili kwa nyakati tofauti na kulazimika kuishi
na wadogo zake wote ndipo alipopata kazi Mackey House kisha akaenda
masomoni Australia.
"Alikuwa ni mtu mwenye msimamo aliitetea
kweli, muadilifu tangu udogo wake hapa alipokufa alipenda sana yatima,
alijali wajane na wastaafu," alisema. Askofu Mhogolo ameacha mjane,
watoto watatu na wajukuu kadhaa.
Via>>Habarileo
Social Plugin