KUTOKA TFF LEO- TFF YAAFIKI UAMUZI WA KAMATI YA MAADILI

TFF YAAFIKI UAMUZI WA KAMATI YA MAADILI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limekubaliana na uamuzi uliofanywa na Kamati ya Maadili katika malalamiko mawili ambayo iliyawasilisha mbele yake, hivyo haitakata rufani.

Katibu Mkuu wa TFF aliwasilisha mashauri mawili mbele ya Kamati hiyo iliyoongozwa na William Erio. Malalamiko ya kwanza yalikuwa dhidi ya waamuzi wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Oden Mbaga na Samwel Mpenzu na wakufunzi wa waamuzi Riziki Majala na Mchungaji Army Sentimea.

Wote aliwalalamikia kwa kuwafanyisha mitihani (wakufunzi), na waamuzi kufanya mitihani hiyo kinyume na utaratibu pamoja na kughushi matokeo.

Kamati katika uamuzi wake iliiagiza waamuzi hao kufanya upya mtihani huo katika robo inayofuata ambapo wakifaulu waendelee kuchezesha mechi. Waamuzi wa FIFA hufanya mitihani hiyo mara nne kwa mwaka.

Kwa upande wa shauri dhidi ya Ofisa Takwimu wa TFF, Sabri Mtulla ambaye alilalamikiwa kwa kuidanganya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuwa hakukuwa na pingamizi dhidi ya mchezaji Emmanuel Okwi, Kamati iliagiza suala hilo liwasilishwe upya pamoja na ushahidi wa kuthibitisha malalamiko hayo.

AZAM, YANGA KUTIMULIANA VUMBI VPL
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Aprili 9 mwaka huu) huku timu za Azam na Yanga ambazo zipo nafasi mbili za juu zikiendelea kuchuana.

Azam itakuwa mgeni wa Ruvu Shooting katika mechi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi mkoani Pwani. Nayo Yanga itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar katika Uwanja wa Taifa jijini.

Yanga, Azam, Ruvu Shooting na Kagera Sugar zote zimeshinda mechi zao za raundi ya 23 wakati mechi za kesho zitakuwa kwa ajili ya kukamilisha raundi ya 24 ya ligi hiyo ambayo inatarajia kukamilika Aprili 19 mwaka huu.

Ligi hiyo itaingia raundi ya 25 Aprili 12 na 13 mwaka huu ambapo timu zote 14 zitakuwa viwanjani. 
 
Aprili 12 mwaka huu itakuwa Mtibwa Sugar vs Ruvu Shooting (Manungu, Morogoro), Coastal Union vs JKT Ruvu (Mkwakwani, Tanga), na Tanzania Prisons vs Rhino Rangers (Sokoine, Mbeya).

Aprili 13 mwaka huu ni Mgambo Shooting vs Kagera Sugar (Mkwakwani, Tanga), Simba vs Ashanti United (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Mbeya City vs Azam (Sokoine, Mbeya) na Oljoro vs Yanga (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha).

TIMU TATU FDL ZARUDI LIGI YA MKOA
Timu tatu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zitacheza Ligi ya Mkoa katika mikoa yao msimu ujao baada ya kushika nafasi za mwisho katika makundi yao, hivyo kushuka daraja.

Transit Camp imekata nafasi ya mwisho katika A wakati Mkamba Rangers imeshuka daraja kwa kukamata mkia katika kundi B. Nayo Pamba SC imerudi kucheza Ligi ya Mkoa wa Mwanza baada ya kuwa ya mwisho kwenye kundi C.
Timu zilizopanda daraja kutoka FDL kwenda Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao ni Ndanda SC ya Mtwara kutoka kundi A, Polisi Morogoro ya kundi B na Stand United ya Shinyanga iliyoibuka kinara katika kundi C.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post