MAMIA WAJITOKEZA KUMZIKA ALIYEKUWA MKUU WA WILAYA KALAMBO MOSHI CHANG'A MKOANI IRINGA

Wakuu wa wilaya na wananchi  Iringa  wakiwa  wamebeba mwili wa Dc Chang'a mjini Iringa leo
WAZIRI wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia leo  amemwakilisha  waziri  mkuu Mizengo Pinda katika mazishi  ya  aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa Marehemu Moshi Chang'a.

Katika mazishi  hayo yalihudhuriwa na mamia  ya  wakazi  wa Manispaa ya  Iringa na viongozi  wa serikali  kutoka mikoa mikoa  mbali mbali nchini pia  spika  wa  bunge Anne Makinda  alitumia nafasi hiyo  kuueleza  umma siri  nzito  iliyofichika  dhidi yake ya marehemu Chang'a mwaka 1995 wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza  ulioshirikisha vyama  vingi kuwa bila marehemu huyo asingeweza kuwa mbunge kutokana na kubanwa na chama cha upinzani cha NCCR Mageuzi kwa  kipindi  hicho

"Mimi  nimekuwa kwa niaba yangu mwenyewe na  jimbo la Njombe  kusini ambalo mimi ni mbunge  wake ....mwaka  1995 marehemu  alikuwa ni katibu  wa CCM Njombe na ndio mwaka  ambao  mfumo wa vyama  vingi  ulianza na yeye ndie  alikuwa katibu  na jimbo hilo  upinzani  ulilizingira kweli na hata kwa kukanyanga mguu kulikuwa hakuna  ila bila Chang'a kweli jimbo  hilo   niseme ukweli  lingekuwa limechukuliwa na Upinzani na kwa kipindi hicho chama chenye nguvu zaidi  kilikuwa ni NCCR Mageuzi "

Akizungumza   wakati wa kutoa  salama  mbali mbali kwa  viongozi  mjini  Iringa Spika Makinda  alisema  kuwa kwa mara ya kwanza  mwaka 1995  alibanwa kupita  kiasi na  NCCR Mageuzi  katika jimbo lake la uchaguzi la Njombe kusini na  kuwa  bila marehemu  huyo ambae kwa kipindi  hicho alikuwa ni katibu wa CCM wilaya ya Njombe kamwe asingeweza kuwa mbunge .

Mkuu wa  mkoa  wa Rukwa injinia Stella Manyanya  alisema kuwa  mkoa  wake amempoteza  kiongozi mzalendo na aliyependa kazi yake na kuwa hata  akiwa  safarini hakuwa na shaka na utendaji kazi wa mkuu  huyo wa  wilaya na kuwa  siku  zote mbali ya kuongoza kama kiongozi wa serikali ila wakati mwingi alitumia  kuwahubiria upendo  wananchi wa  wilaya  yake.

Kwani  alisema kuwa alikuwa hawezi kuanza mkutano  bila kumhubiri  mwenyezi Mungu mbali ya kuwa  yeye alikuwa muumini wa dini ya Kiislam ila alikuwa akihubiria dini ya kikristo  .

Hata  hivyo  alisema kuwa  hadi  kesho anaamini  alishinda  ubunge  jimbo hilo mwaka 1995 si kwa uwezo wake  bali  alishinda kwa uwezo wa marehemu Chang'a ambao  alionyesha  uwezo mkubwa  wa kumnadi na hata kufanikiwa  kuwa mbunge wa  jimbo hilo na leo  kuwa  spika wa bunge .

Alisema  iwapo  angekwama  kuwa  mbunge  mwaka 1995  basi yawezekana leo asingekuwa spika kwani angekuwa amekata tamaa ama angekuwa mbunge  mwingine katika jimbo hilo.

Aidha  alisema mbali ya  kushinda  ubunge  wake bado  wapinzani  walikwenda mahakamani kupinga matokea  ila Chang'a alisimama   na makada  wenzake  wawili moja akiwa ni marehemu  sasa katika kumtetea mahakamani kwa miaka  minne  yote na mbali ya hujuma  kubwa zilizokuwa zikifanywa na Halmashauri ya Njombe kwa kuharibu  baadhi ya nyaraka  za ushahidi ili kuwawezesha NCCR Mageuzi kushinda kesi hiyo japo kwa Chang'a walishindwa kutokana na kuwa na nyaraka  hizo kwa mwenendo mzima wa mchakato  wa uchaguzi huo hadi mahakama  ilipompatia ushindi yeye kama mbunge halali wa jimbo hilo.

" Leo nafanya kazi hii ya uspika kwa kuwa Chang'a ndie  aliyeniweka hapa na bila  yeye  kujituma  mimi  nisingesimama hapa kama spika ....jamani nasema  tuendelee  kujituma katika kazi zetu kama alivyofanya marehemu Chang'a nasema kila mmoja atapimwa utendaji kazi wake hapa duniani "

Kwa  upande  wake  mkuu wa  mkoa wa Mbeya  Abas Kandoro  akimuelezea  Chang'a wakati wa kutoa  salam  hizo  alisema  kuwa  kamwe  hata  sahau utendaji kazi wa mkuu  huyo wa wilaya  ambae amepata  kufanya nae kazi katika wilaya ya Makete ambapo  yeye akiwa mkurugenzi Chang'a alikuwa ni kiongozi wa  CCM wilaya  hiyo  na baada ya kwenda Mbeya  pia  Chang'a amefanya kazi kama mkuu wa wilaya katika mkoa  huo  .

Kandoro alisema kuwa  utendaji  kazi na utumishi  uliotukuka wa  Chang'a ni mfano  wa  kuigwa kwa watumishi wengine wa umma katika Taifa  hili.

Mkuu  wa  mkoa  wa Iringa Dr Christine Ishengoma  alisema kuwa mkoa  wa Iringa  umepata  pigo kubwa kwa  kifo cha mkuu  huyo wa wilaya  hasa ukizingatia mchango mkubwa wa kimaendeleo ambao amepata  kuonyesha ndani ya mkoa na nje ya mkoa na kuwa kamwe  mkoa  utaenzi yote aliyoyaacha .

Mbunge  wa  jimbo la Iringa mjini mchungaji Peter Msigwa  alisema kuwa  wananchi wa Manispaa ya Iringa na mkoa  wa Iringa  tumeendelea  kupoteza  wakuu wa wilaya na kuwa mbali ya Chang'a pia  tumepata  kumpoteza mkuu wa wilaya ya Tabora  na kuwa viongozi hao  wote ni pengo kubwa kwa Taifa .

Mbunge Msigwa alisema kuwa akiwa kama mbunge wa jimbo hilo la Iringa mjini na kiongozi wa Chadema  wilaya  hiyo amepokea kwa masikitiko kifo hicho na kuwa sote kama viongozi  tunapaswa kuangalia ni barua gani ambayo inaachwa kwa jamii baada ya kuondoka na kuwa Chang'a alikuwa ni kiongozi asiyependa  kumchukia mtu na  kila wakati alikuwa ni mtu wa kucheka na kila mmoja.

Awali  akiwasilisha  salama  za  serikali waziri  Ghasia  alisema kuwa  kifo  hicho  kimeacha pengo  kubwa na kumtaja marehemu Chang'a katika mkuu wa wilaya wa mfano  ambae hakupenda  kukataa wala kuonyesha kupinga kwa sehemu  yeyote anayopangiwa kwenda kuwakilisha  wananchi .


Viongozi  wengine  waliopata  kushiriki katika mazishi hayo ni pamoja na viongozi  msaidizi wa Rais Jakaya Kikwete katika masuala ya siasa Ikulu Rajab Luhwavi pia viongozi kutoka mkoa wa Mwanza , Singida ,wabunge  wa bunge la jamhuri ya muungano  akiwemo mbunge wa  viti maalum mkoa  wa Iringa Ritta Kabati na Lediana Mafulu (CCM) naibu  waziri wa maliasili na utalii Mahamudu Mgimwa ambae  pia ni mbunge wa  jimbo la Mufindi kaskazin,baadhi ya  wajumbe wa bunge la katiba  kutoka mkoa  wa Iringa na wakuu wa wilaya mbali mbali akiwemo mkuu wa wilaya ya Kibondo Venance Mwamwoto mkuu wa  wilaya ya Iringa Dr Letisia Warioba ,mkuu wa wilaya ya Kilolo Gerald Guninita  na wengine  wengi .

Na Francis Godwin

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post