Siku chache tu baada ya kutokea mauaji ya watu watano katika eneo la mpaka wa mkoa wa Shinyanga na Tabora kufuatia mapigano kati ya wakulima na wafugaji kutoka wilaya ya Kishapu na Igunga,wakuu wa mikoa hiyo wameunda tume ya watu 18 ili kuchunguza chanzo cha mgogoro wa kugombea ardhi kati ya wakulima na wafugaji ambao umesabisha viofo na uharibifu wa makazi na watu.
Kufuatia mauaji hayo kamati za ulinzi na
usalama za mikoa ya Shinyanga na Tabora zikiongozwa na wakuu wa mikoa hiyo,jana
zilikaa katika kijiji cha Magogo ambako vurugu hizo zimetokea na kuazimia
kuundwa kwa tume ya watu 18 ili kuchunguza chanzo cha mgogoro huo.
Wakitoa taarifa baada ya kikao
hicho, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ally Nassoro Rufunga na Mkuu wa Mkoa wa Tabora
Bi Fatuma Mwasa walisema serikali imelaani vikali vitendo hivyo vilivyofanywa
na wafugaji wa jamii ya Kitaturu na kusema ni vitendo visivyovumilika kwani
siyo desturi ya Watanzania na kwamba serikali imetoa salamu za pole kwa wafiwa
na itahakikisha majeruhi mmoja anahudumiwa.
Wakuu hao wa mikoa walisema pamoja na
kuundwa tume ya kuchunguza chanzo cha mgogoro huo pia kikao hicho kimeazimia
kuwa wafugaji walioko katika kijiji cha Magalata wilayani Kishapu mkoa wa
Shinyanga wabaki kwenye eneo lao na wasivuke mto Manonga kulisha ng'ombe wao na
kwamba
wakulima walioko katika vijiji vya Magogo
na Isakamaliwa wilaya ya Igunga mkoani Tabora wabaki huko na wasivuke mto
Manonga.
Aidha walisema kwa upande wa wakulima
walioharibiwa makazi yao waendelee na shughuli zao kama kawaida katika vijiji
vya Magogo na Isakamaliwa mkoani Tabora na kuongeza kuwa ulinzi wa wananchi wa
vijiji vya Magogo na Isakamaliwa umeimarishwa kwa kuongeza askari polisi ili
kuhakikisha usalama wa eneo hilo unakuwepo.
Kikao pia kimeazimia waharibifu wa makazi
ya watu na wauaji wakamatwe ndani ya siku saba na kwamba halmashauri zote
mbili za Igunga na Kishapu zihakikishe zinaboresha sheria ndogo ili kuwaadhibu
wanaokiuka utaratibu wa mipaka.
Katika hali ya kusikitisha Jumamosi wiki
iliyopita kulitokea mapigano ya wakulima na wafugaji katika kijiji cha
Isakamaliwa kilichopo mpakani mwa wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga na wilaya
ya Igunga mkoa wa Tabora na kusababisha watu watano kupoteza maisha baada ya
kuchomwa mikuki wakati wakigombea mipaka ya malisho na eneo kwa
ajili ya kilimo.
Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya wafugaji walisema mapigano
hayo yametokana na wakulima kulima mazao maeneo yote na kusababisha
wao kukosa maeneo ya malisho na kwamba, pindi wanap kwenda kuchunga mifugo
hunyang’anywa na wakulima huku wafugaji nao wakieleza kuwa siku hiyo baada ya ng’ombe
zaidi ya 3000 kuswagwa na wakulima na kupelekwa wilaya ya Igunga kwa madai kuwa
mifugo inaingia kwenye mashamba yao na kula mazao,kitendo hicho kiliwakera
wafugaji na ndipo mapigano hayo yaliibuka na
kusababisha vifo vya watu watano sambamba na kuharibiwa kwa makazi ya watu.
Social Plugin