Watu wawili wamefariki dunia mkoani Shinyanga katika
matukio mawili tofauti likiwemo la mwanamke mmoja kuuawa kwa kucharangwa
mapanga akiwa nyumbani kwake na watu wasiojulikana na tukio la pili likiwa ni
kijana kuuawa kwa kupigwa mawe baada ya kutuhumiwa kuiba baiskeli.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Evarist
Mangalla amesema tukio la kwanza limetokea Aprili 3 mwaka huu,saa kumi jioni,
ambapo mwanamme mmoja asiyejulikana kwa jina,kabila wala makazi yake mwenye
umri kati ya miaka 25 hadi 30 aliuawa kwa kupigwa mawe kisha mwili wake
kuchomwa moto na wananchi waliojichukulia sheria mkononi katika kijiji cha
Usanda wilaya ya Shinyanga vijijini.
Amesema wananchi hao walifanya mauaji hayo baada ya
kumtuhumu kijana huyo kuiba baiskeli aina ya Sancos Sindelela ambayo haijajulikana thamani yake
wala mmiliki wake.
Kamanda Mangalla amesema baada ya wananchi hao kufanya
mauaji hayo wananchi hao waliondoka na kutokomea na baiskeli hiyo
kusikojulikana.
Kamanda Mangalla amesema tukio la pili limetokea hilo limetokea Aprili 3 mwaka huu
saa mbili asubuhi katika kijiji cha Zumve,kata ya Nindo,wilaya ya Shinyanga
vijijini ambapo mwanamke mmoja ameuawa baada
ya kukatwa kwa panga kichwani,paji la uso na shingoni na watu wasiojulikana
akiwa nyumbani kwake.
Amemtaja mwanamke aliyeuawa kuwa ni Sophia Malandu
mwenye umri kati ya miaka 50 hadi 55.
Kamanda Mangalla amewaasa wananchi kutojichukulia
sheria mkononi na kuwataka kutoa ushirikiano ili kuwabaini na kuwakamata
wahusika wa mauaji hayo.
Social Plugin