Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, James Lembeli (CCM), amesema kuwa
yuko tayari kufanyiwa lolote na chama chake lakini kamwe hatatengua
msimamo wake wa kudai Serikali ya Tanganyika.
Kauli hiyo nzito ya Lembeli, mmoja wa wabunge wa CCM wenye msimamo
mkali, ilipata kutolewa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere miaka ya 90 wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo
chama hicho kilikuwa kikituhumiwa kwa rushwa na hivyo kupoteza mwelekeo.
Katika mazingira hayo, Mwalimu alisema kama chama hicho
kisipojirekebisha, anaweza kurudisha kadi yao, kwani CCM haikuwa mama
yake.
Akizungumza na gazeti la Tanzania daima katika mahojiano maalumu huku akitumia
maneno hayo ya Mwalimu, Lembeli ambaye pia ni Mbunge wa Kahama alisema
baadhi ya wajumbe ni waoga na wanafiki kwa kuogopa kusimamia kile
wanachokiamini.
“Historia haikarabatiwi, mimi naweza kufa au kuadhibiwa na chama changu kutokana na msimamo huu lakini historia itaandikwa.
“Pale Ikulu si kuna picha ya hayati Oscar Kambona, huyu si alifungwa
kwa makosa ya uhaini, mbona picha yake haikuondolewa katika viongozi wa
historia ya nchi hii?” alihoji.
Lembeli alidai kuwa Watanzania wasubiri wamuone wakati wa mjadala wa
pamoja wa rasimu ya Katiba bungeni huku akitamba kuwa hatabadili msimamo
hata kama unakinzana na wenzake wa CCM.
“Sina wa kumfurahisha zaidi ya wapiga kura wangu, hawa ndio wenye
uwezo wa kunishughulikia endapo nitaunga mkono jambo ambalo litakuwa
kinyume na wao.
“Mimi ndiye Lembeli na nitabakia kuwa hivyo, ndiyo maana nilikuwa
nataka itumike kura ya siri ili kuhifadhi uhuru wa mawazo yetu. Nyerere
alituambia kuwa wananchi wanataka mabadiliko na wasipoyapata ndani ya
CCM watayatafuta nje ya CCM,” alisisitiza.
Lembeli aliwataka wajumbe wenzake kuacha woga wa kufungwa na misimamo
ya vyama au makundi yao kwani hata Rais Jakaya Kikwete aliwahi kusema:
“Akili za kuambiwa changanya na zako.”
Via>>Tanzania daima
Social Plugin