Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBUNGE WA CCM JAMES LEMBELI ATOA KAULI NZITO,ASEMA YUKO TAYARI KUFANYIWA LOLOTE NA CHAMA CHAKE,KAMWE HATOBADILI MSIMAMO WAKE KUDAI SERIKALI YA TANGANYIKA,AJIFANANISHA NA NYERERE

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, James Lembeli (CCM), amesema kuwa yuko tayari kufanyiwa lolote na chama chake lakini kamwe hatatengua msimamo wake wa kudai Serikali ya Tanganyika.

 
Kauli hiyo nzito ya Lembeli, mmoja wa wabunge wa CCM wenye msimamo mkali, ilipata kutolewa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere miaka ya 90 wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo chama hicho kilikuwa kikituhumiwa kwa rushwa na hivyo kupoteza mwelekeo.

Katika mazingira hayo, Mwalimu alisema kama chama hicho kisipojirekebisha, anaweza kurudisha kadi yao, kwani CCM haikuwa mama yake.

Akizungumza na gazeti la Tanzania daima katika mahojiano maalumu huku akitumia maneno hayo ya Mwalimu, Lembeli ambaye pia ni Mbunge wa Kahama alisema baadhi ya wajumbe ni waoga na wanafiki kwa kuogopa kusimamia kile wanachokiamini.

“Historia haikarabatiwi, mimi naweza kufa au kuadhibiwa na chama changu kutokana na msimamo huu lakini historia itaandikwa.

“Pale Ikulu si kuna picha ya hayati Oscar Kambona, huyu si alifungwa kwa makosa ya uhaini, mbona picha yake haikuondolewa katika viongozi wa historia ya nchi hii?” alihoji.

Lembeli alidai kuwa Watanzania wasubiri wamuone wakati wa mjadala wa pamoja wa rasimu ya Katiba bungeni huku akitamba kuwa hatabadili msimamo hata kama unakinzana na wenzake wa CCM.

“Sina wa kumfurahisha zaidi ya wapiga kura wangu, hawa ndio wenye uwezo wa kunishughulikia endapo nitaunga mkono jambo ambalo litakuwa kinyume na wao.

“Mimi ndiye Lembeli na nitabakia kuwa hivyo, ndiyo maana nilikuwa nataka itumike kura ya siri ili kuhifadhi uhuru wa mawazo yetu. Nyerere alituambia kuwa wananchi wanataka mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,” alisisitiza.

Lembeli aliwataka wajumbe wenzake kuacha woga wa kufungwa na misimamo ya vyama au makundi yao kwani hata Rais Jakaya Kikwete aliwahi kusema: “Akili za kuambiwa changanya na zako.”
Via>>Tanzania daima

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com