Mwenyekiti wa Chama cha wafugaji Kanda ya Ziwa Bwana Mrida Mshota
aliwasihi wafugaji wa kijiji cha Magalata kutulia na kusubiri taratibu
za serikali |
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa
Ally Nassoro Rufunga amewataka wafugaji wanaoishi katika kijiji cha Magalata
wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kutovuka mto Manonga na kuingia
katika wilaya ya Igunga wakati serikali
inashughulikia suala la mpaka wa wilaya hizo mbili.
Mheshimiwa
Rufunga ametoa agizo hilo jana alipokutana na wafugaji hao katika
kijiji cha Magalata wilayani Kishapu, ikiwa ni moja ya makubaliano ya
kikao cha Kamati za ulinzi na usalama za mikoa ya Tabora na Shinyanga
kilichoketi juzi kuwa kila upande kwa wilaya za Kishapu na Igunga wananchi waelimishwe kutumia ardhi na kuwa watulivu
wakati huu serikali inapofanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha mgogoro
na kufuatilia mpaka halali wa eneo
hilo.
Awali
wafugaji waliieleza kamati ya Ulinzi na Usalama ambayo Mkuu wa mkoa ni
mwenyekiti, kuwa mpaka halisi ni mto Mwanyerere (Manonga) lakini mto huo
ulihama kutokana na mvua mwaka 1998 na sehemu kubwa uliingia eneo la
Kishapu hivyo eneo lao la kitongoji cha Magogo likabaki upande mwingine
na wamekuwa wakichungia huko kwa muda mrefu hadi hapo wakulima wa wilaya
ya Igunga walipovamia eneo hilo ndipo vurugu zilianza.
Naye
Mwenyekiti wa Chama cha wafugaji Kanda ya Ziwa Bwana Mrida Mshota
aliwasihi wafugaji wa kijiji cha Magalata kutulia na kusubiri taratibu
za serikali kwani suala hilo limeanza kushughulikiwa muda mrefu tangu
serikali ilipopata taarifa za uvamizi huo, chama cha wafugaji pia
kinashirikiana kwa karibu na serikali kuhakikisha haki inapatikana.
Mgogoro
huo unatokana na kugombea eneo kati ya wakulima wa kijiji cha
Isakamaliwa wilayani Igunga mkoani Tabora ambao ni wahitimu wa vyuo
vikuu waliopewa eneo hilo na serikali ya
mkoa ya Tabora kwa ajili ya kujiajiri kwa njia ya kilimo, wakati huohuo
wafugaji wa kijiji cha Magalata wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga
wenye asili ya Kitaturu wakidai wamevamiwa eneo hilo kwani wamelisha
mifugo yao kwa miaka mingi hapo.
Serikali
ya Mkoa wa Shinyanga na Tabora zinaendelea kushughulikia tatizo hilo
lililosababisha vifo vya watu watano na majeruhi mmoja ambapo tume ya
watu 18 imeshaundwa na kupewa muda wa wiki nne kufanya uchunguzi wa
chanzo hasa cha mgogoro huo na kujua mpaka halali wakati wananchi wakiendelea
kuelimishwa kuwa na subira.
Na Magdalena Nkulu -Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Shinyanga
Social Plugin