WATU watatu wameripotiwa kufariki dunia jijini Dar es Salaam katika matukio tofauti, akiwamo mke wa Polisi aliyefariki dunia kwa kujinyonga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alimtaja mke huyo wa askari kuwa ni Mayasa Abdallah (43), mkazi wa Kiwalani Minazi Mirefu.
Alisema Mayasa ambaye alikuwa mke wa askari mwenye namba D 2220 Sgt Madukwa wa Polisi Kawe alikutwa amejinyonga chumbani kwake kwa kutumia shuka alilotundika kwenye kenchi.
Alisema sababu za kujinyonga bado hazijafahamika kwa kuwa marehemu hakuacha ujumbe wowote.
Kwa mujibu wa Minangi, mumewe alidai enzi za uhai wake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili. Maiti imehifadhiwa Hospitali ya Amana kwa uchunguzi.
Wakati huohuo, dereva wa pikipiki, Abdalla Furaha (28), mkazi wa Manzese, amefariki dunia baada ya kugongwa na gari T 945 BRL Toyota Coaster, lililokuwa likiendeshwa na dereva ambaye hakufahamika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema ajali hiyo ilitokea juzi, saa 12 asubuhi wakati dereva wa gari hilo akitokea Ubungo kuelekea Kimara alipomgonga dereva huyo aliyekuwa akiendesha pikipiki T 306 CQY Fekon.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni baada ya dereva wa Toyota Coaster kuacha njia na kugongana na pikipiki hiyo uso kwa uso. Maiti imehifadhiwa Hospitali ya Mwananyamala, polisi wanaendelea kumsaka dereva wa gari hilo.
Katika tukio jingine, Hamad Mohamed (34), mkazi wa Mwananyamala Mchangani, mfanyabiashara wa magazeti amefariki dunia baada ya kugongwa na gari, juzi, saa 12 asubuhi, eneo la Vijana, Barabara ya Mwinjuma. Maiti imehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala.
Social Plugin