NB-Hawa ni sungusungu kutoka kata ya Masengwa wilaya ya Shinyanga siyo wa Geita |
Askari wa jadi maarufu kama sungusungu wa mtaa wa Mwatulole kata ya Kalangalala mjini Geita wanadaiwa kumdhalilisha na kumfanyia ukatili mwanamke mmoja kwa kumkamata na kumcharaza viboko kwa tuhuma za kuvaa nguo fupi (kimini).
Inadaiwa kuwa walichukua uamuzi huo baada ya kamanda wao kuwaamuru na kutangaza sheria binafsi ya kuzuia watu kuvaa vimini kwenye mtaa huo.
Akizungumzia kwa masitikiko mwanamke huyo, Jennifa Nobo (24) alidai kuwa alishambuliwa na sungusungu hao Aprili 15, mwaka huu katika mtaa huo wakati amekwenda sokoni.
Jeniffa alisema kuwa alipokwenda sokoni hapo kununua mahitaji ya nyumbani kwake, alikutana na sungusungu hao wakiwa wameongoza na kamanda wao huyo, Daud Kulola.
Alidai baada ya kukutana nao, walimkamata, kumpapasa maungoni wa kumhoji sababu za kuvaa kimini ndani na juu khanga wakati kiongozi wao amepiga marufuku kuvaa mavazi hayo katika mtaa huo.
Jeniffer alidai bila kusikilizwa utetezi wake, sungusungu hao walianza kumcharaza viboko hadharani na kumfuata kila alikokuwa akimbilia.
Alidai wakati wakicharaza viboko walimbakiza na kimini hicho Aliendendelea kudai kuwa kamanda huyo alipochoka kumuadhibu, alimrejeshea khanga yake.
''Nilipita kila kona akanifuata na kunicharaza kwa fimbo nililia sana na kutokwa na haja ndogo kwa hofu na kipigo ..kilikuwa kitendo cha kinyama ambacho sijawahi kutendewa katika maisha yangu na, sitakisahau, ''alidai..
Baadhi ya wakazi wa mtaa huo walidai kuwa siku moja kabla ya tukio hilo la ukatili, Kamanda huyo alisikiska akitumia kipaza sauti akitangaza kuwa vijana na wasichana wote wake kwa waume wanaovaa vimini ni marufuku kuonekana mtaani.
Walidai wengi wao walidhani huenda lilikuwa ni agizo la Serikali.
Baada ya tukio hilo Jeniffa alikwenda kutoa taarifa kituo cha polisi cha Geita kufunguliwa jalada GE/RB/2033/ 2014 la shambulio la kudhuru mwili kisha kupatiwa PF3 kwa ajili ya kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Geita.
Alisema baadaye polisi walimkamata kamanda huyo wa sungusungu na kuachiwa kwa dhamana na kwamba uchunguzi dhidi yake unaendelea.
Kamanda huyo alikataa kuzungumzia madai hayo dhidi yake.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa huo, Kalori Malicery amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kukataa kuzungumzia kwa undani kwa madai limeripotiwa polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alionyesha kusikitishwa na tukio hilo na kuahidi kuzungumzia leo ofisini kwake.
Konyo alisema kuwa iwapo ushahidi utathibitika mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani.
via>>Nipashe
Social Plugin