MWENYEKITI WA CCM -UK MAINA OWINO AJIUZULU WADHIFA WAKE

 
Mwenyekiti wa CCM UK Ndugu Maina Ang'iela Owino jana ametangaza rasmi nia yake ya kujiuzulu Uongozi wa CCM Tawi la UK baada ya kutumikia toka mwaka 2007.
Ndugu Owino alitoa uamuzi huo wa hiari wakati akifungua rasmi kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Tawi la UK kilichokaa Jumamosi tarehe 12/04/2014 katika jiji la Reading, Berkshire, Uingereza.

Ndugu Owino aliwakumbusha wajumbe kuwa awali aliomba kukitumikia Chama kwa muhula mmoja wa uongozi na alitaja kumbukumbu ya vikao vya Chama vilivyomuomba aendelee kukisimamia Chama hasa baada ya kuchaguliwa viongozi wakuu wapya wa Tawi mwezi septemba 2012 jijini Manchester. 
 
Ndugu Owino aliwakumbusha mafanikio waliyopata katika muda wa uongozi wake ikijumuisha harakati za kufungua mashina hadi 15 katika miji na Jiji mbalimbali; Kuhamasisha na kujenga mtandao wa kuanzisha Jumuiya ya kwanza ya Watanzania hapa UK na Kuwashirikisha wanaCCM kuanzisha miradi ya kujitegema ikiwepo ari ya kumiliki jengo la CCM UK.

Alikumbusha pia juhudi na msukumo wa kutaka CCM Taifa kuanzisha dawati rasmi la matawi ya nje na kuyapa uwakilishi wa kudumu katika vikao vya juu vya CCM Taifa. 
 
Pia kupigania Sera ya CCM ya Diaspora iboreshwe kwa Kuanzisha Kituo Maalum cha Diaspora nchini Tanzania ili serikali iwashirikishe na kuratibu hoja na haja za wana Diaspora.
 
Aidha aliwataka wajumbe kutoa ushirikiano wa wazi kwa Idara ya uenezi ambayo kwa sasa inajenga Website ya kisasa na Online TV itakayowapa wanaCCM uhuru wa kutoa maoni na hoja zao bila uwoga lakini kwa nidhamu na kufungua soko la kutangaza bidhaa za Tanzania.

Ndugu Owino alisema wanaCCM hujenga umoja wa kweli na hawaogopi kusingiziwa au kusemwa vibaya na hivyo wasiogope changamoto mbalimbali wakati wanatekeleza Mapinduzi ya umma na kukijenga Chama hapa Uingereza. 

Ndugu Owino aliiomba Halmashauri Kuu ya Tawi ishirikiane na Sekretariati ya Halmashauri Kuu ya Tawi kufanya maandalizi na kupanga tarehe ya Mkutano Mkuu wakati wowote kuanzia sasa ili wanaCCM wote wawe huru kumchagua kiongozi atakaye sukuma CCM UK toka hapa tulipofikia.

Wakati huohuo Halmashauri Kuu ya CCM ya Tawi la UK jana iliazimia kwa pamoja kumsimamisha Katibu wake wa Tawi Mariam Mungula baada ya majadiliano ya kina ya kutokuridhishwa kabisa na utendaji na uratibu wake wa kazi.
 
 Kikao hicho kilipeleka shauri lake kwa Kamati ya Maadili na Usalama ili apate haki ya kujitetea ni kwa nini asiachishwe moja kwa moja kazi yake za Ukatibu wa CCM UK. Ndugu Leybab Mdegela anakaimu nafasi yake kuanzia jana 12/04/2014.

Kikao kiliendelea na hoja zake za kuboresha Chama hapa UK na kuweka mikakati yenye mawazo chanya katika kukisaidia chama katika mikakati kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wote wa Tanzania.

Imetolewa na 
Abraham Sangiwa  
Idara ya Itikadi na Uenezi ya Halmashauri Kuu ya CCM UK.  
13/04/2014.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post