Ikiwa ni chache tu baada ya kutokea
mauaji ya watu watano na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa wakati wa mapigano ya wafugaji na wakulima katika eneo la
mpaka kati ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na Igunga mkoani Tabora kutokana na mgogoro wa ardhi,imeelezwa kuwa ugomvi
huo pia umetokana na wananchi kugombania maji ya mto Manonga uliopo katika eneo hilo.
Akizungumza juzi kwenye mkutano wa hadhara na wafugaji wa kabila la Kitaturu
wilayani Kishapu naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini Kaika Telele baada ya kutembelea
eneo la mgogoro huo na kujionea jinsi machafuko yalivyotokea alisema kila upande
umekuwa ukiutupia lawama upande wa pili kwamba wao ndiyo wakorofi.
Alisema baada ya kukutana na pande zote mbili na kuzungumza nao
amebaini kwamba sababu nyingine ya kutokea kwa mgogoro huo ni wananchi kugombania
maji ya Mto Manonga uliopo katika eneo hilo ambapo wakulima na wafugaji
wamekuwa wakivutana.
“Wakulima wanatumia maji ya Mto
Manonga kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji wamekuwa wakidai kuwa wafugaji wanachafua maji
hayo kwa kujaza vinyesi vya ng’ombe,na wafugaji nao wanadai kuwa wakulima
wanatumia maji mengi kumwagilia mashamba yao na hivyo kuna hatari ya kukosa
maji ya kunyweshea mifugo yao”,alifafanua waziri Telele
Waziri Telele baada ya kutembelea eneo hilo la mgogoro na kuzungumza na
pande zote mbili za wakulima wa Igunga na wafugaji wa Kishapu ambapo kila
wilaya imekuwa ikisema eneo hilo ni lao, ataunda tume ya wataalamu kulichunguza
tatizo la mgogoro huo pamoja na kupima hekali ya eneo lote na kuligawa
katikati.
“Tarehe 4 mwezi huu nimeongea na
wafugaji wa Igunga kuhusu eneo hilo na leo naongea na nyie wafugaji wa Kishapu,na
kila upande unasema upo sahihi kutumia eneo la mpaka huo,suala hili nalichukua
na nitaliundia tume ya wataalamu ili kufika katika eneo la mgogoro kwa kupima
eneo lote na kuligawa kisheria kila wilaya ipate upande wake”,alisema Telele
Aidha alizitaka kamati za ulinzi na
usalama za pande zote mbili ziendelee kuimarisha ulinzi wa maeneo yao na
kuwatuliza wananchi wazingatie maelekezo ya kutovuka Mto Manonga mpaka hapo
Serikali itakapo tatua tatizo hilo kisheria ilikuzuia machafuko yasitokee tena.
Naye mwenyekiti wa wafugaji katika kijiji cha
Magalata wilayani Kishapu Jidonye Majuluga alisema tume hiyo inatakiwa kuundwa haraka
iwezekanavyo ikiwezekana ndani ya mwezi huu kwani wakulima bado wanavuka mto
huo na kuingia katika eneo la wafugaji hivyo machafuko ya uvunjifu wa amani
yanaweza kutokea tena muda wowote.
Social Plugin