KIMENUKA! Jeshi la Polisi Tanzania kwa kushirikiana na taasisi
mbalimbali za serikali zimeanza kuwachunguza watu wenye majina makubwa
‘mastaa’ Bongo ambao wameibuka na utajiri wa ghafla, Uwazi limeambiwa.
Kwa mujibu wa chanzo nyeti ambacho kiko ‘jikoni’ kwenye jeshi hilo,
mbali na mastaa, wengine ambao tayari orodha yao ipo ni wafanyabiashara,
wafanyakazi wa serikali na viongozi wa dini ambao wameibuka kuwa
mamilionea kwa muda mfupi huku shughuli zao za wazi zikiwa haziwezi
kuwatajirisha.
Chanzo: “Imeonekana kuwa mastaa wengi wanaibuka kuwa na utajiri siku
hizi, huenda wanajihusisha na kusafirisha madawa ya kulevya.
“Ndiyo maana wengi wao kila kukicha, mara wapo China, mara India,
wengine wanakwenda mpaka Thailand. Hao wanachunguzwa kwa mtindo wa
nyendo, kila mmoja ambaye yumo kwenye orodha ya jeshi amewekewa askari
wawili wa kumfuatilia.”
KUKAMATWA
Chanzo hicho kikaendelea kusema kuwa
wale ambao watathibitika kwamba biashara zao za wazi haziwezi kutoa
utajiri wa ghafla watakamatwa na kuhojiwa.
Chanzo hicho kilieleza kuwa katika oparesheni hiyo maalum, watu kumi
wameshakamatwa, akiwemo Mtangazaji wa Kituo cha Redio cha Times FM,
Hadija Shaibu ‘Dida’.
“Watu kumi tayari wamekamatwa na kuhojiwa.
Yumo yule mtangazaji Dida wa Mchops (siku hizi si wa Mchops). Saba
wamekwenda na maji, watatu akiwemo Dida waliachiwa baada ya kuthibitika
kwamba mali zao ni halali,” kilisema chanzo.
IKOJE KWA VIONGOZI WA DINI?
Chanzo kilisema kuwa
kuhusu viongozi wa dini ambao nao wameibuka kuwa matajiri wa kutupwa,
wamejenga mahekalu ya maana, nao wanachunguzwa na kati ya watu kumi
waliokamatwa, yumo mchungaji mmoja (hakumtaja jina) ambaye aliachiwa.
“Lakini orodha ya hawa ni ndefu, kumbe wengi wanajihusisha na kuuza
madawa ya kulevya. Nao wamewekewa askari wawiliwawili ambao wanaingia
hadi kwenye ibada zao lakini wenyewe hawajui,” kilisema chanzo.
JOTI WA KOMEDI ATAJWA
Katika hali ya
kushangaza, chanzo hicho kilidai kuwa staa ambaye alikuwemo kwenye
orodha na akafuatiliwa na kuachiwa ni msanii wa Kundi la Orijino Komedi,
Lucas Mhuvile ‘Joti’ ambapo ilidaiwa hakuonekana kuwemo kwenye cheni ya
wauza unga nchini.
“Lakini hata hiyo orodha nyingine si kwamba wamehukumiwa kuhusika
kufanya biashara hiyo ila wanachunguzwa,” kilisema chanzo hicho.
YAMEKUJAJE?
Hatua hiyo, kwa mujibu wa chanzo,
imekuja kufuatia madai ya wananchi wengi kwamba matajiri waliopo mtaani
wengi ni wauza unga ambao hufanya biashara hiyo waziwazi, wengine
wakisema kuna polisi wanaojua kila kitu lakini kwa sababu wanakatiwa
kitu kidogo wanawalinda.
“Si kwamba serikali haitaki watu wawe na maendeleo makubwa, bali
utajiri wao uwe wa wazi wenye vielelezo vinavyokubalika. Kwa sasa vijana
wengi wakiwemo wasanii na wachezaji wanashindana kwa utajiri lakini
baadhi yao ndiyo hivyo tena wamegundulika wanajihusisha na biashara ya
madawa ya kulevya, wengine wamekamatwa nje ya nchi na wanakabiliwa na
hukumu ya kifo,” kiliongeza chanzo hicho.
UWAZI LAWASAKA WALIOIBUKA NA UTAJIRI
Kama kigezo
kikubwa ni utajiri wa ghafla, Uwazi liliwasaka mastaa ambao
walishaandikwa na Magazeti Pendwa ya Global Publishers (likiwemo Uwazi
lenyewe).
DIDA
Katika Gazeti la Ijumaa Wikienda toleo la
wiki mbili nyuma kulikuwa na kichwa cha habari ukurasa wa mbele; UTAJIRI
WA DIDA GUMZO.
Katika habari hiyo Dida alisema:
“Mimi sipendi kuanika vitu ninavyomiliki ila ni kweli nina nyumba
mbili, moja Kigamboni na nyingine Goba ya gorofa. Magari ninayo matatu,
hilo Vogue mchakato unaendelea, ukikamilika nitaliingiza nchini.
“Kuhusu miradi yangu mingine siwezi kuianika hadharani kwa sababu, kwanza sipendi kabisa mambo hayo.”
Hata hivyo, Dida alikiri kukamatwa Machi, mwaka huu na kuhojiwa kisha kuachiwa. Alikuwa anakwenda Hong Kong, China.
Katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko la Jumatano ya Aprili 2, 2014
ukurasa wa mbele kulikuwa na kichwa cha habari; UTAJIRI WA MASANJA
KUFURU.
Masanja alipoulizwa alikoupata utajiri huo alisema: “Ni kweli nina
nyumba tatu hapa mjini, kampuni ya ulinzi na mashamba ya mpunga ekari 50
nyumbani Mbarali, Mbeya. Kuhusu magari pia ni kweli kabisa. Mimi ni
mtumishi sitakiwi kusema uongo. Orijino Komedi ndiyo chanzo cha vyote,
pale ndipo kwenye koki.”
Katika Gazeti la Ijumaa Wikienda toleo la Julai 29, 2013 ukurasa wa mbele kuliandikwa; DIAMOND ANUNUA MTAA.
Diamond (Nasibu Abdul) alipoulizwa alikiri na kusema: “Muziki ndiyo
chanzo kikubwa. Najua (nyumba) zitanisaidia endapo muziki wangu utakosa
soko. Mimi na mama yangu (Sanura Kassim ‘Sandra’) tuliishi kwa dhiki
sana na sasa kwa kipindi hiki ambacho Mungu ananisaidia na kuniwezesha
kupata fedha kwa wingi, siwezi kuishi maisha ya anasa ya kununua magari
ya kifahari bali najenga nyumba.”
Kwa upande wake, Kajala ambaye aliwahi kuandikwa na Gazeti la Amani
likiwa na kichwa; KAJALA AIBUKA TAJIRI GHAFLA, alipoulizwa alisema:
“Sina utajiri wa ghafla bali namtegemea Mungu, natengeneza filamu naweka pesa ndiyo maana naweza kufanya makubwa.”
Staa wa filamu Bongo, Muhsin Awadh ‘Dk. Cheni’ hakupatikana katika simu na marafiki zake walisema yupo safarini nchini China.
VICKY KAMATA
Huyu ni Mbunge wa Viti Maalum
(UVCCM), Geita. Aliandikwa na Gazeti la Uwazi la Februari 18, mwaka huu
kwa kichwa; UTAJIRI WA VICKY KAMATA BALAA.
Katika mahojiano na Uwazi kuhusu utajiri wake, Vicky alisema:
“Mafanikio yote yametokana na juhudi zangu za kujituma katika kufanya
kazi, namwamini Mungu siku zote. Hakuna dhambi mbaya hapa duniani kama
kukata tamaa. Tukifanya kazi kwa kujituma na kumwamini Mungu hakuna
Mtanzania maskini.”
Mchungaji Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima yeye aliandikwa
kwa kuchanganywa na utajiri wa wenzake wengine. Lakini alipohojiwa
alisema:
“Mali nilizonazo ni kutokana na jitihada zangu kwani mimi ni mwalimu,
nimekuwa nikisafiri kwenda nchi za Ulaya kufundisha na huwa nalipwa
fedha nyingi, pia mali zingine ikiwemo gari la Hummer nilipewa na
marafiki zangu, mali zingine ni za kanisa.”
Katika Gazeti la Uwazi la Desemba 11, 2012, Lusekelo Anthony ‘Mzee wa
Upako’ wa Kanisa la Maombezi, aliandikwa kwa kichwa; UTAJIRI WA MZEE WA
UPAKO NI KUFURU.
Alipohojiwa, alisema: Magari yote nimeandika kwa jina langu ili niyalipie kodi, situmii mwamvuli wa kanisa kwa kukwepa kodi.
“Kila mtu anatakiwa kuwa tajiri lakini utajiri wa halali siyo ule wa
kudhulumu, ndiyo maana naweza kusimama hapa madhabahuni na kutaja mali
zangu, magari hayo si mali ya kanisa ni yangu.”
KAMANDA NZOWA
Uwazi lilimsaka Kamanda wa Kikosi
cha Kupambana na Kuzuia Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa ambapo
alikiri kuwachunguza watu wengi ambao majina yao yamepelekwa na
wananchi au wametajwa na watuhumiwa wengine ambao wameshakamatwa.
“Hapa tuna majina ya watu wengi wa aina mbalimbali wakiwemo viongozi
wa dini, wasanii, viongozi wa serikali na wafanyakazi wa taasisi za
serikali na zisizo za serikali. Hawa ni wale ambao wameibuka kuwa
matajiri ghafla.
“Siwezi kukutajia majina yao kwa sababu mambo haya yanafanyika kwa
siri kwani hawa watu ni wajanja sana, kwa sasa vita hii si yangu tu bali
ni ya task force, wananchi na dunia kwa jumla, kwa kweli kuna orodha
ndefu na hili zoezi si la muda mfupi ni endelevu,” alisema Kamanda
Nzowa.
GPL
Social Plugin