Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RUSHWA YA NGONO YAMPA PRESHA MEYA WA MWANZA

Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula amekemea vikali tabia ya baadhi ya mameneja na wateja wa hoteli kuomba rushwa ya ngono kwa wahudumu.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa Umoja wa Wafanyakazi wa Hoteli Kanda ya Ziwa (LHA) juzi, Mabula alisema suala la rushwa ya ngono ni kikwazo cha maendeleo kwa sekta ya utalii.

“Lengo la LHA ni kuliangalia tabaka la chini kwanza, halafu ndiyo mjiangalie mameneja, kwani mkiheshimu sekta hii muhimu kwa pato la nchi, nasi tutafuata,” alisema na kuongeza kuwa mameneja ni vijana wenye nguvu, wenye malengo na waliodhamiria kukomboa sekta hii kwa kuwathamini watu ambao ni tabaka la chini, kwa kukomesha rushwa ya ngono.

“Yapo masuala yanayowahusu wanataaluma, sisi tunapaswa kuheshimu na kuthamini taaluma zao kama wanataaluma wenyewe watajithamini na kujitambua. Tunafahamu changamoto zinazowakabili ila naahidi Serikali inawaunga mkono kwa yale mazuri mnayoyafanya,” alisema.

Mabula alisema sekta ya hoteli ina changamoto nyingi, ikiwamo uchache wa watumishi wenye maadili, hoteli zenye hadhi ya nyota tano kwa kuwa wakipata wageni 1,000 hatuwezi kuwamudu kwa ubora wa viwango..

Naye Katibu wa umoja huo, Shijani Mtunga alisema lengo lao ni kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao za msingi kama kutambulika kisheria.

“Kongamano la utalii la Februari liligusa suala la kuongeza hoteli, kudumisha ufanisi na kuongeza ushindani, lakini haya yote yanawezekana kama mameneja na wamiliki wataacha kuwanyanyasa wafanyakazi ‘‘alisema Mtunga.

Mwenyekiti wa LHA, Dharmesh Talsania alisema lengo lao lilikuwa kupata washiriki kutoka hoteli 30 kati ya 180 zilizopo mkoani hapa, hata hivyo waliofanikiwa kusimamisha umoja huo wakiwa na hoteli 17.

via>>Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com