Baadhi
ya wananchi mjini Shinyanga wameulalamikia uamuzi wa hospitali ya serikali
mkoani humo kuongeza gharama za matibabu na kuanzishwa kwa huduma maalumu kwa
watu wenye fedha maarufu kwa jina la Fast Track na kutaka uamuzi huo utazamwe
upya kwani itawafanya wasio na uwezo wakimbilie kwa waganga wa kienyeji.
Malalamiko
ya wananchi hao yanatokana na uongozi wa hospitali hiyo kutangaza kuanza kutumika
kwa viwango vipya vya matibabu kuanzia leo Aprili mosi, ambapo huduma ya
cheti itatolewa kwa gharama ya shilingi 5,000/= badala ya bei ya zamani ya
shilingi 1,000/= na gharama za kitanda itakuwa pia shilingi 5,000/= kwa wiki.
Wakazi
hao wa Shinyanga walisema ongezeko la gharama za matibabu litachangia kwa kiasi
kikubwa wananchi wasio na uwezo kushindwa kwenda hospitali na badala yake
kurejea enzi za ujima kwa kukimbilia kwa waganga wa kienyeji.
“Kwa
kweli pamoja na kwamba jamii tunapaswa kuchangia gharama za matibabu kama
ilivyo sera ya afya hapa nchini, lakini ongezeko la kutoka shilingi 1,000/=
hadi shilingi 5,000/= halikuzingatia hali halisi ya kipato cha mtanzania kwa
hivi sasa, wengi tutashindwa kutibiwa maana hata mishahara yetu haijaongezwa”,alisema
mmoja wa wananchi hao aitwaye Joseph Hamis.
“Ni
vizuri uongozi wa hospitali yetu ukaliangalia suala hili vinginevyo watu
watashindwa kwenda kupata huduma za matibabu katika hospitali ya serikali na
kuanza kujitibu kienyeji au mitaani ambako huduma zake si salama sana, kila
siku tunasikia zahanati za watu binafsi zinavyofungiwa kutokana na ukiukwaji wa
taratibu,” aliongeza.
Naye Khadija Kassim alisema uanzishwaji wa huduma ya
matibabu ya haraka kwa watu wenye fedha utatengeneza matabaka ya walionacho na
wasiokuwa nacho katika kupata huduma za afya kwa vile ni wazi watu wenye fedha
ndiyo watakaopewa kipaumbele zaidi na kushauri kusitishwa kwa mpango huo mara
moja.
“Kuanzisha
utaratibu wa Fast Track katika hospitali ya umma kutasababisha matatizo
makubwa, maana madaktari wetu wataweka kipaumbele zaidi katika kuwashughulikia
watu wenye fedha na sisi masikini tutabaguliwa, hii ni hatari ni vizuri mpango
huu ukasitishwa, isije kuwa mfano wa tuisheni shuleni,” alisema Khadija.
Akijibu
malalamiko hayo kaimu mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Maguja Daniel
alikiri kuanza kutumika kwa viwango vipya vya matibabu katika hospitali yake
hali iliyosababishwa na ongezeko la gharama za uendeshaji ikiwemo kuporomoka
kwa thamani ya shilingi ya Tanzania na kwamba uamuzi huo una baraka zote za
bodi ya hospitali.
Kuhusu
utaratibu wa huduma ya haraka (fast track) itakayokuwa na malipo ya shilingi
10,000/= kwa ajili ya cheti, alisema hautaathiri matibabu kwa wagonjwa wengine
wa kawaida kwa vile huduma hiyo itatolewa baada ya muda wa kawaida wa saa za
kazi saa 9.30 mchana na haitokuwa nyakati za asubuhi.
“Ni
kweli kuanzia Aprili Mosi ,2014 huduma zote za matibabu katika hospitali yetu
zimepanda kuanzia pale mtu anapochukua cheti kwa ajili ya kwenda kuonana na
daktari itakuwa ni shilingi 5,000/= badala ya shilingi 1,000, akilazwa shilingi
5,000/= kwa siku saba, upasuaji mdogo sasa ni shilingi 40,000/= na mkubwa
shilingi 80,000/=,”
“Kwa
upande wa vipimo vidogo vya kawaida kama vile B/S, choo ndogo na kubwa itakuwa
shilingi 2,000/= badala ya shilingi 300/=, tohara shilingi 40,000/=, ushonaji
majeraha machache shilingi 20,000/=, michubuko shilingi 10,000/= ambapo kwa
atakayepasuliwa jipu atatozwa shilingi 40,000/=,” alieleza Dkt. Daniel.
Hata
hivyo alisema viwango hivyo ni kwa hospitali hiyo ya mkoa ambayo ni ya
rufaa kwa ngazi ya mkoa na kwamba ni vyema wakazi wa mjini Shinyanga wakajenga
utaratibu wa kuanzia kupata matibabu katika hospitali za manispaa ambako pia
kuna huduma zote na inaposhindikana ndipo waende katika hospitali hiyo.
Social Plugin