Shinyanga Leo- SASA MARUFUKU KUZIKIA NYUMBANI

Diwani wa kata ya Ndembezi katika manispaa ya Shinyanga David Nkulila(pichani),ambaye pia ni naibu meya wa manispaa ya Shinyanga amewataka wakazi wa kijiji cha Ndembezi kilichopo katika kata yake kuepuka kufanya shughuli za mazishi wanafamilia kwenye maeneo ya nyumba zao na badala yake wafanye shughuli hizo katika eneo la makaburi lililotengwa kutokana na kwamba hivi sasa Ndembezi siyo kijiji hivyo kutakuwa na mitaa.


Akizungumza wakati wa kikao cha kamati ya maendeleo ya kata hiyo kilichofanyika leo katika ukumbi wa ofisi ya afisa mtendaji wa kata hiyo,Nkulila amesema  ni vyema wananchi wakafuata utaratibu uliowekwa na viongozi.

"Ndugu zangu naomba tuwakumbushe wananchi wetu waache kufanya mazishi nyumbani,kijiji hiki kimefutika kwa mujibu wa taratibu,sasa Ndembezi ni mjini,siyo kijiji tena,kutakuwa na mitaa,machinjio ya kisasa na tayari zoezi la kupima viwanja lilishaanza,wananchi wakazike kwenye makaburi",aliongeza Nkulila.

Diwani huyo alisema Ndembezi sasa  ni mjini kama lilivyo eneo la  Stendi mjini Shinyanga.

Alisema ni vyema sasa wananchi wakaelimishwa kuhusu mabadiliko hayo ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea siku zijazo mfano mtu akiamuriwa kuhamisha kaburi la ndugu yake kutokana na kuzika  mahali pasipostahili.

Kikao hicho cha kamati ya maendeleo ya kata ya Ndembezi kimeazimia viongozi wa taasisi za kidini katika eneo hilo kuandikiwa barua kuelekeza waumini kuhusu matumizi mazuri ya makaburi.

Kikao hicho pamoja na mambo mengine pia kimeazimia kupanga kikao kingine cha dharura kwa ajili ya kusoma taarifa kuhusu mgogoro wa uendeshaji ujenzi wa choo cha shule ya msingi Bugoyi B iliyopo baada ya mamlaka iliyopewa jukumu la kufanya ukaguzi kumaliza kazi yake.
Diwani wa kata ya Ndembezi David Nkulila,aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho alisema kutokana na upekee na uzito wa jambo hilo,kamati ya maendeleo ya kata hiyo itaitisha kikao cha dharura kwa ajili ya kutoa taarifa ya ukaguzi katika shule hiyo. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post