MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) imepiga marufuku vipodozi 222, baada ya kugundulika kuwa vina viambata vyenye sumu.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Alananga.
Analanga alisema kuwa vipodozi hivyo vimepigwa marufuku baada ya
kufanyika kwa uchunguzi wa kimaabara ambapo uchunguzi huo umegundua
kuwepo kwa viambata 11 vyenye sumu vinavyoweza kusababisha madhara kwa
binadamu.
“Mpaka sasa tuna viambata 11 vya kisayansi ambavyo tumevichunguza na
kugundua kuwa vina madhara kwa mtumiaji. Tumegundua karibu vipodozi 222
nchini vina viambata hivyo,’’ alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo TFDA inadhibiti uingizwaji na
usambazaji wa vipodozi hususan kwenye mipaka rasmi kwa kuweka mawakala
wa mamlaka hiyo kwa ajili ya kupima vipodozi vinavyoingizwa kwenye
mipaka hiyo.
Alisema kuwa moja ya vipodozi vyenye sumu ambavyo ni changamoto
kuvidhibiti ni mafuta ya Carolite ambayo hutumiwa na watu wengi licha ya
kuwa na madhara ambayo ni ya muda mfupi na mrefu.
Aliyataja madhara ya muda mfupi yanayotokana na kipodozi hicho ni
muwasho, kutokea kwa mabaka meusi ambapo madhara ya muda mrefu ni kansa
ya ngozi ambayo hutokea baada ya sumu kujikusanya taratibu.
Madhara
mengine ni watoto kuzaliwa wakiwa na mtindio wa ubongo.
Analanga alitoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara wanaouza na
kuagiza vipodozi salama pamoja na kuonana na wataalamu wa TFDA ili
kuhakiki vipodozi hivyo.
Social Plugin