Wananchi wa kijiji cha Bugulula katika kata ya Bugulula wilayani Geita mkoani Geita wamemtaka mwenyekiti wa kijiji hicho bwana Bahati Matati kulirudisha shamba lao walilokuwa wakilitumia kwa ajili ya maziko kwa kujimilikisha na kuanza kulilima mihogo kwa ajili ya manufaa yake mwenyewe.
Wakiongea kwa nyakati tofauti jana na waandishi wa habari waliofika kijijini hapo na kushuhudia mgogoro huo wamesema kuwa wanashangaa kuona mwenyekiti wa kijiji hicho anachukua shamba hilo lililotengwa na wananchi kwenye mkutano wa serikali ya kijiji kwa ajili ya maziko na kumshangaa mwenyekiti huyo kuona analilima mihogo .
Wananchi hao wameongeza kuwa kitendo cha mwenyekiti huyo kupora shamba hilo na kujimilikisha kwa ubabe si cha kiungwana na ni cha kinyume kabisa hivyo kuomba serikali ya juu kuweza kuriludisha eneo hilo kwa wananchi na liendelee na kazi iliyokusudiwa kwa kuwa ni sehemu ya maziko.
Mwananchi mmoja ambaye hakuta jina lake litajwe alisema wamekuwa wakimwambia mwenyekiti huyo kurudisha shamba hilo na badala ya kurudisha shamba anawabambikizia watu kesi mbaya.
"Ndugu mwandishi shamba hili mwenyekiti katupora kipindi alipoingia madarakani ,alikaa na serikali yake bila kutushirikisha wananchi ,wakatoa maamuzi na tukashitukia ameshaanza kulilima bila ya kufahamishwa hivyo unavyoona hata wiki mbili zilizopita kuna mtu amefariki tukaenda kumzika humo humo kwenye mihogo maana sisi bado tunajua ni eneo letu halali’’,alisema.
Baada ya malalamiko hayo kutolewa na wananchi , mwandishi wa habari hii alimtafuta mwenyekiti huyo Bahati Matati na kutaka kujua kama hizo tuhuma ni za kweli,ambapo alisema shamba hilo ni la kwake na alipewa na uongozi wa wa serikali ya kijiji baada yakuingia madarakani awamu hii.
Aliongeza kuwa kuna wananchi wana chuki naye kwa kuona anamiliki shamba kama hilo na kwamba kuna eneo lingine amelitenga kwa ajili ya maziko lakini alishangaa juzi wananchi walikwenda kuzika kwenye shamba lake.
Kuhusu kubambikizia wananchi kesi alisema siyo kweli.
Na Valence Robert -Geita.