UCHAGUZI wa serikali za mitaa, ambao hufanyika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu, huenda usifanyike mwaka huu, imeelezwa.
Hatua hiyo inatokana na uchaguzi huo kuingiliana na masuala ya kupata Katiba mpya, ambayo mchakato wake bado unaendelea.
“Nikiri nafasi ni finyu sana ila tutalizungumza serikalini,” alisema Rais Jakaya Kikwete, alipozungumza na baadhi ya wahariri Ikulu mjini Dar es Salaam juzi.
Rais Kikwete alisema atakutana na viongozi wengine wa serikali ili kuamua kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa kama ufanyike mwishoni mwa mwaka huu kama ilivyo kawaida au la.
Alisema ni kweli nafasi ya kufanyika kwa uchaguzi huo ni finyu sana kwa kuwa suala la Katiba mpya litaendelea hadi mwishoni mwa mwaka huu kipindi ambacho uchaguzi huo huwa ukifanyika.
Iwapo uchaguzi huo utaahirishwa, huenda ukafanyika mwakani na uchaguzi mkuu, lakini tofauti na ilivyozoeleka, upigaji kura utakuwa nne kwa Tanzania Bara.
Kwa kawaida upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu unahusisha kura ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kura kwa ajili ya mbunge na kura ya diwani.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kueleza wasiwasi wake kuhusu kuahirishwa kwa uchaguzi huo.
Pinda aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma hivi karibuni kuwa, muda uliopangwa kwa ajili ya Bunge Maalum ni siku 70, lakini kazi ilikuwa ikienda kwa kusuasua.
“Hatari ya kusogeza mbele uchaguzi wa serikali za mitaa ninaiona dhahiri, nadhani itabidi tu tumuombe Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, tusogeze mbele uchaguzi huu, ili kutoa nafasi kwa kazi zingine kuendelea hususan ya kutengeneza katiba,” alisema Pinda.
Pinda alisema pia kuwa iwapo kazi ya bunge hilo itakuwa haijamalizika ifikapo mwishoni mwa Aprili mwaka huu, watamuomba Rais Kikwete aliahirishe ili lipishe Bunge la Bajeti liendelee na kazi zake.
“Hatuwezi kuacha kazi zingine za serikali zikasimama, lazima ziendelee, na zitaendelea kama bajeti za wizara zitapitishwa, nadhani kama hatutakwenda sawa, tutamuomba tu Rais aahirishe bunge hili la Katiba, tufanye kazi hii nyingine iliyo mbele yetu,” alisema Pinda.
Credit: Gazeti la Uhuru