Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Ukatili Kahama-!MZEE AUAWA KWA KUSHAMBULIWA KWA SILAHA ZA JADI,KISA KUIBA MAHINDI MABICHI KWENYE SHAMBA LA MTU




Mtu mmoja Hamisi Mayala anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 58 hadi 60 amefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa silaha za jadi na wananchi waliojichukulia sheria mkononi katika kijiji cha Kilago wilayani Kahama Mkoani Shinyanga baada ya kumtuhumu kuiba mahindi mabichi kwenye shamba la mtu. 

Akizungumza na Redio Kahama Diwani wa Kata ya Kilago Peter Emanuel amesema tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 12 jioni baada ya baadhi ya wananchi kumkuta akivunja mahindi katika shamba ambalo halijafahamika kuwa ni la nani. 

Amesema wananchi hao baada ya kumkuta akiiba mahindi hayo walipiga kelele ndipo umati wa watu ukajaa na kuanza kumshambulia kwa silaha za jadi hadi kuumuua na kwamba wananchi walisambaa baada ya kuona mtuhumiwa huyo amepoteza maisha. 

Diwani Emmanuel amesema amepata taarifa kutoka kwa viongozi wake wa kijiji, na kuchukua jukumu la kupiga simu Polisi ambao wamefika jana asubuhi na kuruhusu mwili wa marehemu uzikwe kwa kuwa ndugu zake wahakufahamika mara moja. 

Amesema Marehemu Mayala ameingia kijijini hapo mwaka Juzi na alikuwa anaishi katika nyumba ya kupanga huku akijishughulisha na kufanya vibarua kwa wakulima wa kijiji hicho na inadaiwa alitokea katika Tarafa ya Msalala Wilayani Kahama. 

Hata hivyo Diwani Emmanuel amewataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake wawafikishe watuhumiwa sehemu inayohusika, huku akiahidi kulisaidia jeshi la polisi kutoa elimu kwa wananchi. 

Jeshi la polisi Mkoani Shinyanga limethibitisha kutokea kwa tukia hilo na linaendelea na Uchunguzi wa kuwabaini waliohusika na mauaji hayo ya kujichukulia sheria mkononi na kuwafikisha katika mikono ya sheria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com