NB-Picha haiendani na habari |
Mtoto Aisha Selemani (6), mkazi wa kijiji cha Liputu kata ya Mwena ya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, amejeruhiwa vibaya kwa kuchomwa kwa kisu cha moto sehemu zake ya siri ya haja kubwa.
Kitendo hicho kinadaiwa kufanywa na mama yake wa kambo baada ya mtoto huyo kujisaidia haja kubwa kwenye nguo alizokuwa amevaa.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea mwishoni mwa wiki na uongozi wa kijiji hicho umethibitisha.
Mmoja wa ndugu wa mtoto huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema mama wa mtoto huyo alitengana na baba yake muda mrefu.
Alifafanua kuwa baada ya kutengana, mtoto huyo aliendelea kuishi na mama yake eneo la Uwanja wa Ndege jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, alisema baba yake aliamua kumfuata mwanawe Dar es Salaam na kumtorosha kwa mama yake, aliyetajwa kwa jina moja la Agness na kuja kumkabidhi alelewe na mama yake wa kambo hapa Masasi.
Lakini alidai kuwa mtoto huyo amekuwa akiteswa na mama huyo wa kambo kwa kupigwa, kunyimwa chakula na kulazimishwa kulala sakafuni.
“Nilibaini hali hiyo baada ya mtoto huyo kuja kuomba moto nyumbani kwangu, ndipo nilipoona jeraha kubwa mguuni na baada ya kumuuliza alisema alichomwa na mama yake na aliendelea kunionyesha majeraha mengine sehemu za makalio za haja kubwa,” alidai.
Aliongeza kuwa mama huyo wa kambo alifikia hatua ya kutumia vifaa vyenye ncha kali kama vile nyembe kumjeruhi mtoto huyo kwenye makalio yake na baadaye alimweka pilipili kwenye majeraha hayo mazingira ambayo yalimsababishia aishi na maumivu makali.
Naye Sista Letisia OSB wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye matatizo mbalimbali cha Ndanda ambaye kwa sasa anamhudumia mtoto huyo, alisema kuwa alipata taarifa za mtoto huyo kulazwa hospitalini hapo baada ya kuchomwa moto na mama yake wa kambo na hakuna mtu anayempa msaada.
Sista Letisia alisema kutokana na hali hiyo ndipo alipoamua kwenda kumsaidia mtoto huyo.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mohammed Yassin, alidai kwamba baada ya kupata taarifa za kuunguzwa kwa mtoto Aisha, aliongozana na mtendaji wake kwenda nyumbani kwa baba wa mtoto huyo, Selemani Hamisi.
Alisema walithibitisha kuwa kweli mtoto huyo amechomwa moto na hivyo wakampeleka katika kituo cha polisi.
Hata hivyo, alidai kuwa mama huyo aliachiwa huru kituo cha polisi katika mazingira ya kutatanisha.
Yassin alisema alimpigia simu baba wa mtoto huyo, lakini alikana kutokea hayo na kudai kuwa mkewe anasingiziwa kutokana na wivu wa kipato alichonacho.
Mtoto Aisha kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Ndanda akipatiwa matibabu chini ya uangalizi wa Sista Leticia OSB jirani wa mtoto huyo, Reinfrida Makumbuli.
Baadhi ya majirani akiwamo Reinfrida Makumbuli, walidai kuwa mama huyo amekuwa na tabia ya kumtesa mtoto huyo ikiwamo kumnyima chakula.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Steven, kuzungumzia suala hilo, zilishindikana baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila ya kupokelewa na juhudi za kumtafuta zinaendelea kumtafuta Kamanda Steven ili kupata maelezo ya kina juu ya tukio hilo la kusikitisha.
via>>Nipashe