Vidole vya mtoto Amos Baya kama vinavyoonekana hapo vimevunjwa haviwezi kunyooka
Wakati watu wengine wanakesha kila siku kutafuta watoto lakini pia wadau mbalimbali wakiendelea kupiga vita ukatili dhidi ya wanawake na watoto,lakini vitendo hivyo vimeendelea kujitokeza katika jamii ambapo huko katika kijiji cha Senane wilayani Maswa mkoa mpya wa Simiyu mwanamme mmjoa aitwaye Baya Seni amekuwa akimpa mateso makali mtoto wake
wa kiume mwenye umri wa miaka minne ili afe kwa madai kuwa hapendi watoto wa kiume.
Baya Seni ambaye ni mkazi wa kijiji hicho cha Senane amekuwa akimpa mateso makali mtoto huyo anayejulikana kwa
jina la Amos Baya mwenye umri wa miaka minne toka kuzaliwa kwake hali
iliyoelezwa kusababisha mtoto huyo kudhoofika mwili na kupata ugonjwa wa utapiamlo.
Miongoni mwa mateso aliyoyapata mtoto huyo ni pamoja na kuvunjwa
vidole vya mkono wa kushoto, kutelekezwa shambani siku zaidi ya mbili bila kula
na kuning'inizwa juu ya mti.
Imeelezwa kuwa Mwanamme huyo hapendi watoto wa kiume kwa madai kuwa
wanaleta umaskini kwa sababu wakikua watataka kuoa na kuchukua mali, lakini
mtoto wa kike akikua ataolewa na kuleta mali nyumbani.
Taarifa za mtoto huyo kupata mateso kutoka kwa baba yake mzazi zilitolewa na msamaria
mwema siku ya tarehe 31 mwezi Machi
mwaka huu ambaye alikwenda katika
shughuli za mazishi katika kijiji hicho na kumwona mtoto huyo ndipo akapiga simu ofisi ya ustawi wa
jamii wilaya ya Maswa na kufuatia taarifa hizo ofisi hiyo iliwataarifu polisi na wakaenda
kumchukua mtoto huyo na kumuweka chini ya ulinzi baba mzazi wa mtoto huyo.
Afisa ustawi wa jamii wilayani maswa Bwana Husein Mshana amethibitisha kutokea kwa tukio hilo
Hivi sasa mtoto huyo amelazwa wodi namba nane ya watoto katika hospitali
ya wilaya ya Maswa akipatiwa matibabu.
Mama
mzazi wa mtoto huyo Elizabeth Paul amekiri kuwa mtoto huyo amekuwa akifanyiwa vitendo vya ukatili na baba
yake mzazi na kwamba hata yeye amekuwa akipewa
vitisho kuwa endapo atasema atauawa.
Tayari baba mzazi wa mtoto huyo Amos Baya anashikiliwa na jeshi
la polisi wilayani maswa kwa hatua za kisheria.
Na Veronica Natalis-Simiyu
|
Social Plugin