Watu 11 wamepoteza maisha papo
hapo na mwingine mmoja kufariki dunia akiwa njiani akipelekwa hospitali ya rufaa ya Bugando,baada ya kutokea ajali mbaya
ya gari iliyohusisha basi la abiria la kampuni ya Luhuye T 410 AWQ lililokuwa
likitokea Tarime Mkoani Mara kwenda jijini Mwanza.
Basi hilo liligonga nyumba kisha kupinduka
leo saa tano na dakika 10 asubuhi katika
barabara ya Mwanza – Mara katika kijiji cha Itwilima kata ya Kiloleli wilaya ya
Busega Mkoani Simiyu.
Mbali na watu 12 kufariki dunia pia watu
60 wamejeruhiwa ambapo imeelezwa kuwa chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendo kasi wa sasi hilo ambapo dereva wa alishindwa
kumudu gari hilo likiwa katika kasi na kusababisha kugonga nyumba iliyokuwa
pembezoni mwa barabara na kupinduka.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwemo
wa malunde1 blog katika eneo la tukio, mkuu wa Mkoa wa Simiyu Paschal Mabiti
amesema miongoni mwa abiria waliopoteza maisha katika ajali hiyo wanawake ni 5
na wanaume 7.
Walioshuhudia ajali hiyo wamesema kabla ya
kutokea kwa ajali hiyo basi hilo
lilianza kuyumba na kusababisha kugonga nyumba iliyokuwa kando kando ya
barabara hiyo.
Mganga mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Magu
mkoani Mwanza Dk Athuman Pembe alithibitisha kupokea majeruhi 60 pamoja na miili
11 ya marehemu.
Amesema kati ya majeruhi hao 25 hali zao siyo nzuri wamepelekwa katika hospitali
ya Rufaa Bugando jijini Mwanza, na kwamba hali za majeruhi waliobaki katika
hospitali hiyo zinaendelea vizuri na tayari wengine wameanza kuruhusiwa.
Jeshi la polisi mkoani Simiyu limethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Social Plugin