Wananchi wa
kijiji cha Singita kata ya Usanda wilaya ya Shinyanga vijijini mkoani Shinyanga
wanakabiliwa na uhaba wa maji safi na salama hali inayowafanya kutumia maji ya
mto ambayo pia hutumiwa na wanyama aina ya fisi.
Wakizungumza
juzi na waandishi wa habari baada ya kutembelea kijiji cha Singita kilichopo
katika kata ya Usanda wilaya ya Shinyanga vijijini wananchi hao walisema kwa zaidi
ya miaka hamsini hawapati huduma ya maji safi na salama kwani wamekuwa maji ya
mto Shimiwi ambayo si salama kwa vile hayafai kunywewa.
Wananchi hao
walidai kuwa kwa miaka mingi wamekuwa maji
hayo kwa shughuli mbalimbali kama vile kunywa,kufyatulia matofali , kufuria
nguo na maji hayo pia yanatumiwa na wanyama aina ya fisi.
“Kwa kweli
haya maji si salama kwa afya zetu kwani wakati mwingine tumekuwa tukikuta fisi wamechezea maji hayo na kuacha vinyesi
vyao ndani ya maji”,walisema.
“Kijiji hiki
kina vitongoji kumi na mara kwa mara tumekuwa
tukipewa ahadi na viongozi wetu kuwa watatuletea maji hayo lakini mpaka leo
hakuna lolote hivyo tumeamua kuishi tu na hali yetu kama tulivyo zoea”,Waliongeza.
Kwa upande
wake mwenyekiti wa kijiji hicho Mohamed Jumanne alisema wananchi wake wamekuwa
wakitumia maji ya mto huku wengine wakitumia maji ya kwenye majaruba
wakati wa masika kutokana na maji ya mto kuchafuka na kipindi kwa
asilimia kubwa kwa kuchanganyikana na vinyesi vya wanyama fisi pamoja na
binadamu ambao hujisaidia vichakani.
Jumanne
alisema baadhi ya wananchi wa kijiji hicho kwa asilimia kubwa hutumia maji hayo
kwa matumizi ya kunywa bila ya kuyachemsha hali ambayo huhatarisha afya zao kwa
kukabiliwa na magonjwa hatari yatokanayo na matumizi ya maji.
Afisa afya
wa kata ya Usanda katika kijiji cha Singita Chade Musa na Muuguzi wa Zahanati
wa kijiji hicho Leticia Anthony walisema ni vigumu kubaini idadi ya wagonjwa wanaotokana
na maji hayo machafu kutokana na zahanati hiyo kutokuwa na maabara yenye vipimo
hivyo, huku wakidai na wao hutumia maji hayo ingawa huyachemsha.
Diwani wa
kata ya Usanda Abeid Ndaji kupitia Chama Cha Mapinduzi alikiri kuwepo kwa
tatizo la maji safi na salama katika kijiji hicho ambapo alisema mwaka 2012
serikali iliahidi kuwajengea visima virefu vitatu ili kukidhi mahitaji ya
wananchi hao lakini wamekuwa wakilifuatilia bila ya mafanikio.
Diwani huyo alitumia
fursa hiyo kumuomba waziri mwenye dhamana kufika katika kijiji hicho kujionea
hali halisi ya wananchi hao jinsi wanavyopopata shida ya maji na kuwatatulia
tatizo hilo ambalo limekuwa likiwasumbua kwa kipindi kirefu.
“Tatizo la
maji safi na salama katika kijiji hiki limekuwa sugu tangu nianze kuwa kiongozi
mwaka 1994 kuwa diwani wa kata ya Usanda wananchi hawa wamekuwa wakipata shida
ya maji hayo na nimekuwa nikipiga kelele kwenye baraza la madiwani ndani ya
miaka 20 wananchi wapatiwe maji hayo bila ya mafanikio “ alisema Ndaji.