MBUNGE WA JIMBO LA KAHAMA JAMES LEMBELI
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga kimeeleza kusikitishwa na kauli iliyotolewa na mwanachama wa chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa Kahama, James Lembeli kwamba CCM si mama yake.
Wakizungumza
na waandishi wa habari kwenye ofisi za Makao Makuu ya CCM, viongozi wa
juu wa chama hicho wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga,
Khamis Mgeja, viongozi hao walisema kauli hiyo ni ya kushtua.
“Chama
Cha Mapinduzi Shinyanga kinalaani vikali kauli ya Lembeli aliyoitoa
hivi karibuni na kunukuliwa na vyombo vya habari akisema ‘CCM si mama
yangu’.
“CCM
Shinyanga tumeshtushwa na kauli ya Lembeli anayetokana na CCM, kwani
kauli hii hatukutegemea sote kama ingeweza kutolewa na mwanachama
ambaye tena ni kiongozi ndani ya chama,” alisema Katibu wa Siasa na
Uenezi wa Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Mlimandago.
Alisema
CCM haina tatizo na msimamo wa Mbunge huyo kuhusu msimamo wake wa
serikali moja, mbili, tatu, nne au serikali ya Tanganyika kwani huo ni
uhuru wake binafsi; lakini tatizo ni kauli kuwa CCM si mama yake kwani
ameitoa mahali ambapo si sahihi.
Katibu
huyo wa Itikadi na Uenezi, alisema jambo la ajabu ni kwa Mbunge huyo
kulitumia jina la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere vibaya kwa
kujifananisha na kauli zake wakati akiwa hana hadhi na sifa za Mwalimu
Nyerere.
“Kwa
Lembeli kujifananisha na Baba wa Taifa ni matumizi mabaya ya
kujitwisha sifa asizostahili kwani Mwalimu Nyerere alikuwa na karama,
heshima na busara kubwa za pekee na aliheshimika duniani kote pia
alikuwa anatoa kauli zake kutokana na mazingira yaliyokuwepo wakati
husika,” alisema Mlimandago.
Kwa
upande wake Mgeja, alisema pamoja na kuelezwa kukerwa na kauli hiyo,
CCM itatumia vikao halali katika kujadili kauli hiyo ya Lembeli ili
kuona hatua stahiki zinazoweza kuchukuliwa kulingana na uzito wa kauli
yake hiyo.
Akizungumza
kwa simu akiwa Kahama, Lembeli alisema hawezi kuwazuia
viongozi hao wa CCM Mkoa wa Shinyanga kusema jambo wanalolitaka wao;
kwa vile ni haki yao kutoa maoni yao kama ilivyokuwa haki yake na yeye
kutoa maoni yake kwa jambo lolote.
Social Plugin