Wananchi wa kijiji
cha Mwamashimba kata ya Mwamalasa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga
wamesikitishwa na vitendo vya baadhi ya wajumbe wa bunge la katiba vya kutukana
na kudhihaki waasisi wa taifa na kudai kuwa watu hao wanaokashfu viongozi huenda wana ugonjwa wa
kansa ya ubongo.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti na waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho,wananchi hao
walisema vitendo vya kuwakosea heshima waasisi wa taifa akiwemo baba wa taifa
hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati Amani Abeid Karume siyo vya
kiungwana kwani viongozi hao ndiyo waliolifikisha taifa hapa lilipo.
Walisema kumekuwa
na tabia ambazo siyo za kiungwana tena kinyume na maadili ya kitanzania
zinazofanywa na baadhi ya wajumbe wa bunge la katiba kama vile kudhihaki kazi
waliyofanya waasisi hao kuunganisha nchi mbili Tanganyika
na Zanzibar .
Mmoja wa wananchi
hao aliyejitambulisha kwa jina la Shija Manoni alisema waasisi hao walifanya
kitu kizuri cha kuunganisha nchi mbili kutokana na upeo na ulewa wao na kwamba kama kuna mapungufu basi wangetumia ufahamu na elimu zao
kutatua changamoto za muungano lakini siyo kuuvunja.
“Ndugu
waandishi,unajua kwa mtu mwenye akili timamu kuwapuuza waasisi wa taifa, ni
laana kubwa,waasisi hawa ndiyo waliosababisha tuishi kwa mshikamano,upendo na
amani,na ndiyo walisababisha hata hawa wanaojiita wasomi kupata kupata elimu
wanayayojivunia”,aliongeza Manoni.
Kwa upande wake bi
Malimi John mkazi wa kijiji hicho mwenye umri wa miaka 68 aliyekuwa akiongea
kwa shida kwa lugha ya kisukuma alisema watu wasiojua kusoma walidai uhuru na
waasisi wa taifa,na baada ya kupata uhuru walijiwekea mikakati ya kusomesha
watoto ili waje kuwa wataalamu kuisaidia nchi na matokeo yake wasomi hao
wameanza kutukana wazee.
“Sisi tunashangaa
kusikia wasomi wetu wanadharau waasisi wa taifa hadi baba wa taifa,wakati sisi
tunamweshimu alitutoa mikononi mwa wakoloni,tukawa kitu kimoja,hivi hawa wana
akili timamu kweli,au wana matatizo ya kansa ya ubongo?”,alihoji mama huyo.
Bi John alisema ni
vyema wajumbe wa bunge la katiba wakatumia elimu yao kutatua changamoto za muungano badala ya
kuanzisha ujanja ujanja wa kuvunja muungano kwani muungano ndiyo umelifikisha
taifa hapa lilipo.
via>>Zanzibar Leo
Social Plugin