Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Ajali mbaya Shinyanga!! FUSO YAUA NG'OMBE 7 NA MBUZI PAPO HAPO,MCHUNGAJI AZIMIA

 
Kumetokea ajali mbaya mjini Shinyanga ambapo ng’ombe 7 na mbuzi 1 wamekufa papo hapo baada ya kugongwa na gari aina ya fuso lenye namba za usajiri T .799 BJG likiwa imebeba mawe katika kitongoji cha Mwalugoye kata ya Chibe barabara ya kwenda bwawani katika manipaa ya Shinyanga .


Walioshuhudia tukio hilo wamesema limetokea jana majira ya saa 12 jioni wakati ng’ombe hao wakirudi nyumbani kutoka kwenye malisho ambapo ghafla gari liligonga mifugo zaidi ya 50 mchungaji wa mifugo maarufu kwa jina la Mwanaholo akinusurika kugongwa na kusababisha kuzimia kufuatia ajali hiyo.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo Hamis Nkuba amesema gari hilo likiendesha kwa mwendo kasi liligonga mifugo hiyo iliyokuwa katikati ya barabara na kuhama njia na kwenda vichakani huku lilimkosa kumgonga mchungaji wa mifugo huyo na muda mfupi ng’ombe na mbuzi hao wakianza kufa mmoja baada ya mwingine.


Akizungumza na Malunde1 Blog mwenyekiti wa kitongoji cha Mwalugoye katika kata ya Chibe  kulikotokea ajali hiyo Deus Samike amesema ng’ombe 7 na mbuzi mmoja walikufa papo hapo huku ng’ombe wawili na mbuzi wakijeruhiwa vibaya.

"Mara nyingi magari yamekuwa yakipita kwa kasi sana eneo hili,madereva hawako makini, katika ajali hii mifugo 51 imenusurika kufa,yaani mbuzi 12 na ng’ombe 38”,amesema Samike.

Afisa mifugo  kata ya Chibe John Kisanga amesema baada ya tukio hilo walimkamata dereva na tayari ameshafikishwa kwenye vyombo vya dola.

Amewataja waathirika wa mifugo yao katika ajali hiyo ambao huchanganya ng’ombe kwa pamoja kuwa ni Hamisi Kameja Nkuba Nkuba,Mbonge Mahushi na Kashindye Mahungi.

Kwa upande wao waathirika hao wamesema ajari hiyo imewatia hasara na kuwarudisha nyuma kimaendeleo kwani mifugo hiyo huitumia kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za kilimo. 

Naye afisa mtendaji wa kata ya Chibe Wiliam Ndile amewataka wananchi kutofanya vurugu yoyote juu ya magari yanayopita katika barabara hiyo ili kuendelea kulinda amani ya nchi huku akiongeza kuwa suala hilo limeshafika kwenye vyombo vya sheria na litafanyiwa kazi na waathirika watalipwa fidia ya mali zao.

Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Shinyanga Evarist Mangalla amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Na Kadama Malunde wa Malunde1 blog-Shinyanga





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com