Mahakama ya Wilaya ya Liwale, Lindi imemhukumu Mussa Chande kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka 11 anayesoma darasa la nne Shule ya Msingi Kawawa.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Liwale, Eric Ruhumbiza alimtia hatiani mshtakiwa kwa kosa hilo chini ya Kifungu namba 130 na 131 vya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (Sospa) ya mwaka 1998.
Ruhimbiza alisema Mahakama imeridhishwa na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mlalamikaji mahakamani hapo na kumtia hatiani pasi na shaka yoyote mshtakiwa kwani ushahidi uliotolewa na shahidi namba tano ambaye ni binti aliyebakwa ambaye alitoa maelezo ya maumbile na viungo vya siri vya mtuhumiwa ulitosheleza.
Awali, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, PC Josephat alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 8, mwaka huu saa nne asubuhi ndani ya Msikiti wa Kawawa, Liwale jirani kabisa na shule anayosomea mwanafunzi huyo.
Alisema mshtakiwa alimchukua mtoto huyo na kumwingiza msikitini, sehemu wanayosalia wanawake na kumlaza chini na kumvua nguo huku akimfunika kwa kanga usoni.
Aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa huyo kabla ya kumbaka, alimwekea Kitabu kitukufu cha Quran kichwani na kumwambia kuwa kwa aya anayomsomea, akimweleza mtu kitu atakachomfanyia atageuka kipofu.
Alisema jambo hilo lilifahamika baada ya mfanyabiashara katika na eneo la shule hiyo kutilia shaka nyendo za mwalimu huyo wa dini kuingia kwenye msikiti upande wa wanawake na kutoka kila mara kuchungulia nje.
Alisema mfanyabiashara huyo alipofuatilia, alikuta mwanafunzi huyo akitoka msikitini huku akilia na alipomhoji alimweleza kilichojiri ndipo alipoomba msaada kwa wanawake waliokuwa jirani.
Alisema wanawake hao walimchukua na kumwogesha kisha wakampeleka hospitalini. Alisema uchunguzi ulipofanyika katika eneo la tukio, mbegu za kiume zilionekana pamoja na kanga.
Mwendesha mashtaka aliiomba Mahakama impe adhabu kali mshtakiwa kwani licha ya tendo ovu la kumbaka na kumdhalilisha mtoto huyo, aliudhalilisha Uislamu na kitabu kitakatifu cha Quran kufanikisha uhalifu wake.
Na Mwanja Ibadi, Mwananchi
Social Plugin