AZAM Tv imefanya kufuru kwa kutoa udhamini wa Sh 361.6 milioni kwa ajili ya kurusha ‘live’ mashindano ya mpira wa kikapu ya Miji Mikuu ya Afrika Mashariki na Kati, ambayo yameaanza jana Jumanne Uwanja wa Ndani wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mashindano hayo yatafanyika kwa siku sita kuanzia jana Jumanne mpaka Jumapili, Azam itakuwa inarusha mechi zote kuanzia saa 2 asubuhi mpaka saa 2 usiku mechi hizo zinapomalizika kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo.
Kurusha mechi moja kwa saa moja ni Dola 3,000 (Sh 4.8 milioni) ambapo kwa saa 12 itakuwa ni Sh57.6 milioni na hivyo kwa siku sita ni sawa na Sh345.6 milioni. Imeelezwa kuwa Azam wameahidi kusaidia bajeti ya Sh16 milioni ambayo waandaji walipeleka hivyo kufika kiwango cha Sh 361.6 milioni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Mwenze Kabinda, alisema; “Bajeti yetu ilikuwa ni Sh16 milioni ndiyo tuliyopeleka kuomba kusaidiwa, lakini Azam wamechukua jukumu la kutudhamini kurusha mechi zetu zote na kusaidia fedha tulizoomba. Sisi tusingeweza kufanya hivyo kwani kiasi tulichoomba kilikuwa ni kwa ajili ya maandalizi mpaka tutakapomaliza.”