Breaking News!! SERIKALI YASITISHA HUDUMA YA FAST TRACK KATIKA HOSPITALI YA MKOA WA SHINYANGA

Mbunge wa viti maalum mkoa wa Shinyanga kupitia ccm  Azza Hilal akizungumza kwenye mkutano wa wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Shinyanga na kueleza kutoridhishwa kitendo cha bodi ya afya mkoa wa Shinyanga kupandisha gharama za matibabu katika hospitali ya mkoa ambapo amesema ni kutowatendea haki wananchi
Habari zilizoufikia mtandao huu wa malunde1 blog hivi punde zinasema kuwa serikali ya mkoa wa Shinyanga imesitisha huduma ya fast Track katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga ambako hivi karibuni huduma za matibabu katika hospitali hiyo zilipanda mfano katika kupanda huko kwa huduma za matibabu akina mama walikuwa wanalazimika kujifungua kwa gharama ya shilingi elfu 70,na kama ni ulikuwa unahitaji kupasua jipu  basi ingekulazimu kulipia huduma hiyo shilingi elfu 40,kumwona daktari shilingi 10,000?= na mengine mengi.

Awali akizungumza katika kikao hicho mbunge wa viti maalum 
mkoa wa Shinyanga kupitia ccm  Azza Hilal kwenye mkutano wa wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Shinyanga,aliyetaka kujua imekuwaje gharama za matibabu zikapanda katika hospitali ya mkoa na hospitali hiyo kuwa ya rufaa bila kufuata utaratibu unaotakiwa tena limepitishwa bila kupata baraka za kikao cha baraza la ushauri la mkoa na mkuu wa mkoa wa Shinyanga alibariki kuwepo kwa mabadiliko hayo.

Mbunge huyo alisema suala la kupandisha gharama za matibabu katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga wakati wananchi wake wana kipato duni ni kutowatendea haki wananchi huku akieleza kushangazwa na hatua ya kuwa na hospitali ya rufaa wakati hakuna hospitali ya wilaya.

Kufuatia hoja ya mbunge Azza Hilal ,wajumbe wengine wa kikao hicho nao hawakuwa nyuma kueleza walichokuwa nacho kwenye mioyo yao ambapo walidai kuwa kitendo cha bodi ya afya ya mkoa kupitisha suala la kupanda kwa gharama za matibabu katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga siyo la CCM  huenda ni mawazo ya wapinzani yaliyobarikiwa na mkuu wa mkoa kukidhoofisha chama cha mapinduzi hasa katika kipindi hiki ambapo chama kinaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu na kuongeza kuwa kitendo cha kupandisha gharama za matibabu ni kukifanya chama kichukiwe na wananchi.

Kufuatia  hali tete kuibuka katika kikao hicho mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Nassoro Rufunga alilazimika kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo na malalamiko mengi  yaliyoibuka kuhusu kupanda kwa gharama za matibabu kupanda katika hospitali hiyo wakati wananchi wengi ni maskini ambapo alisema serikali kuanzia sasa imesitisha mchakato huo kwa ajili ya maslahi ya wananchi na chama tawala.

"Bodi ya afya imekosea,sasa tunasitisha kwa muda,huduma za matibabu katika hospitali ya mkoa ziendelee kama zamani,tunasitisha huduma ya fast tarck,hata mimi nilishtushwa na taarifa za kupanda kwa gharama za matibabu,huu utaratibu nausitisha,kesho nitatoa barua/waraka maalum kuhusu suala hili,kweli linaumiza wananchi wetu,nitakaa na bodi hii tuangalie namna ya kushughulika na jambo hili",alieleza Rufunga.

Naye mwenyekiti wa ccm mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho alisema ni vyema watendaji wa serikali wakawa makini na masuala yanayogusa maslahi/maisha ya wananchi kwani lengo la chama cha mapinduzi ni kuwaletea maendeleo wananchi na kutatua kero zinazowakabili.

Mgeja alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa serikali na chama kuendelea kushirikiana katika kuwaletea maendeleo wananchi na kwamba kamwe chama cha mapinduzi hakiwezi kunyamaza kama mambo yanaenda mrama.

Kikao cha wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Shinyanga  kimehudhuriwa na watendaji wakuu wa serikali,wakuu wa wilaya,wakurugenzi wa halmshauri,wenyeviti wa halmashauri za wilaya,mkuu wa mkoa,katibu tawala wa mko,wabunge na wanachama mbalimbali wa ccm.

Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post