Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CCM SHINYANGA YATUMA SALAM ZA RAMBIRAMBI KWA IGP MANGU KUHUSU POLISI ALIYEUAWA JIJINI DAR ES SALAAM

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja

Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga kimetoa salaam za rambirambi kwa  mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu kufuatia kifo cha askari wake namba  E.8850 Koplo Busagara Faustin (35) aliyeuawa na majambazi alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kazi.
 
Salaam hizo zimetolewa juzi na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja wakati wa mazishi ya askari polisi huyo yaliyofanyika kijiji alichozaliwa cha Iselamagazi  wilaya ya Shinyanga vijijini.
 
Mwenyekiti huyo wa CCM alisema msiba huo siyo wa familia pekee bali ni wa taifa zima la Tanzania na kwamba  CCM imeguswa na msiba huo hasa ikizingatiwa marehemu Busagara alipoteza uhai wake wakati akilitumikia taifa lake.
 
Alisema askari huyo alipoteza maisha kutokana na juhudi zake za kupambana na majambazi waliokuwa wamevamia nyumbani kwa mfanyabiashara huko katika mtaa wa Kitomondo wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.
 
“Chama cha Mapinduzi mkoani Shinyanga tunaungana na familia ya marehemu Busagara katika kipindi hiki cha majonzi mazito cha kuondokewa mtoto na ndugu yao kipenzi aliyekuwa katika kutimiza majukumu yake ya kazi za kila siku na pia tunatoa pole kwa askari polisi wote nchini pamoja na IGP Manghu kwa msiba huu mzito,”
 
“Ndugu zangu CCM tuna imani na jeshi la polisi kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kulinda raia na mali zao, tunaamini wale wote walioshiriki katika tukio hilo ambao wamebaki watasakwa popote pale walipo na kukamatwa na hatimaye kufikishwa katika vyombo vya sheria ili waweze kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria,” alieleza Mgeja.
 
Mgeja alitoa wito kwa wananchi wote wapenda amani nchini kujenga tabia ya kujitokeza katika kufichua wahalifu kwani baadhi ya wahalifu hao wanafahamika na wanaishi nao mitaani wengine wakiwa ni watoto wao wa kuzaa na kwamba kuendelea kuwaficha ni sawa na kufuga nyoka ndani.
 
Naye mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum aliwaomba wanafamilia kuwa na subira katika kipindi hiki kizito cha maombolezo na kwamba yeye mwenyewe amesikitishwa na tukio hilo kutokana na ukaribu wake ndani ya familia hiyo ambapo alitoa rambirambi kwa wafiwa kiasi cha shilingi milioni tatu.
 
Akitoa shukrani zake kwa viongozi wa CCM na serikali mkoani Shinyanga, baba mzazi wa marehemu, Masale Sengerema alisema mtoto wao amekufa kishujaa wakati akilitumikia taifa lake na kwamba mbali ya yeye mwenyewe kuuawa lakini alifanikiwa kuua majambazi wawili.
 
Mazishi ya askari polisi huyo pia yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali wakiwemo mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Annarose Nyamubi, mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa, Azza Hillal, mkurugenzi mtendaji Mohamed Kiyungi na madiwani wa halmashauri ya wilaya pamoja wakazi wa kata ya Iselamagazi na vijiji jirani.
 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com