DAKTARI AFARIKI DUNIA AKIWA AMELALA GESTI JIJINI DAR ES SALAAM


MTU mmoja aliyedaiwa kuwa ni daktari wa jijini Mwanza, Raymond Simion (36) amekutwa amekufa ndani ya chumba kwenye nyumba ya kulala wageni ‘gesti’ ijulikanayo kwa jina la Nesta iliyopo Ubungo NHC wilayani Kinondoni jijini Dar. 

 Taarifa kutoka katika gesti hiyo zinasema marehemu alijiorodhesha kwenye kitabu cha wageni kuwa ni daktari wa Hosptali ya Nyamagana jijini Mwanza na alikuja  Dar kikazi kwa muda wa wiki moja. Mauti yalimkuta akiwa na siku mbili tu tangu alipowasili.

 Mmoja wa wahudumu wa gesti hiyo ambaye hakupenda jina lake litajwe alisema kuwa, daktari huyo alifika katika gesti hiyo Jumapili ya Mei 4, mwaka huu na kuchukua chumba namba 102.

Alisema Jumatatu ya Mei 5, marehemu aliomba abadilishiwe chumba, akapewa namba 105 ambamo mauti yalimkutia.


 Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ubungo NHC, Amani Sizian alisema taarifa ya kifo cha daktari huyo aliipokea saa 9: 03 alasiri ya siku ya tukio ambapo mhudumu wa gesti hiyo ndiye aliyempigia simu kumjulisha.

 Kiongozi huyo aliendelea kusema kuwa mhudumu huyo alimweleza kwamba marehemu baada ya kuchukua chumba Jumapili alitoka na kurudi saa 3:00 usiku ambapo alilala, lakini kesho yake hakuonekana kutoka.


 “Mhudumu aliniambia kuwa baada ya kutomwona asubuhi, hawakumfuatilia hadi ilipofika saa 9:00 alasiri ambapo walikwenda kumchungulia chumbani kwake na kumwona katika hali ya kutokuwa hai.

“Ilibidi niende. Nilipofika tukakuta mlango umefungwa kwa ndani.

 Katika kumchungulia tulimwona mtu huyo akiwa amekaa kitandani bila kujigeuza jambo lililonifanya nipige simu polisi ambao walifika na kuvunja mlango na kumkuta akiwa amefariki dunia,” alisema mwenyekiti huyo.

 Aliongeza kuwa, katika chumba hicho alichofia mteja huyo, kulikutwa mabomba mawili ya sindano ambapo moja lilikwishatumika, pia kulikuwa na mifuko miwili yenye nguo na begi moja.

 Polisi waliuchukua mwili na kuupeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili. Hata hivyo, ndugu wa marehemu walipatikana na mwili kufanyiwa uchunguzi na daktari kisha kuuchukua na kuusafirisha kwenda Mwanza kwa mazishi.


 Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Camilius Wambura alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema: “Marehemu alikutwa na mabomba mawili ya sindano, moja lilishatumika na lilikuwa na masalia ya damu. Pia kulikuwa na kete moja ya vitu vinavyodhaniwa kuwa ni madawa ya kulevya.

 >>>UWAZI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post