MTU mmoja aliyedaiwa kuwa ni daktari wa jijini Mwanza, Raymond Simion (36) amekutwa amekufa ndani ya chumba kwenye nyumba ya kulala wageni ‘gesti’ ijulikanayo kwa jina la Nesta iliyopo Ubungo NHC wilayani Kinondoni jijini Dar.
Mmoja wa wahudumu wa gesti hiyo ambaye hakupenda jina lake litajwe alisema kuwa, daktari huyo alifika katika gesti hiyo Jumapili ya Mei 4, mwaka huu na kuchukua chumba namba 102.
Alisema Jumatatu ya Mei 5, marehemu aliomba abadilishiwe chumba, akapewa namba 105 ambamo mauti yalimkutia.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ubungo NHC, Amani Sizian alisema taarifa ya kifo cha daktari huyo aliipokea saa 9: 03 alasiri ya siku ya tukio ambapo mhudumu wa gesti hiyo ndiye aliyempigia simu kumjulisha.
Kiongozi huyo aliendelea kusema kuwa mhudumu huyo alimweleza kwamba marehemu baada ya kuchukua chumba Jumapili alitoka na kurudi saa 3:00 usiku ambapo alilala, lakini kesho yake hakuonekana kutoka.
“Ilibidi niende. Nilipofika tukakuta mlango umefungwa kwa ndani.
Katika kumchungulia tulimwona mtu huyo akiwa amekaa kitandani bila kujigeuza jambo lililonifanya nipige simu polisi ambao walifika na kuvunja mlango na kumkuta akiwa amefariki dunia,” alisema mwenyekiti huyo.
Aliongeza kuwa, katika chumba hicho alichofia mteja huyo, kulikutwa mabomba mawili ya sindano ambapo moja lilikwishatumika, pia kulikuwa na mifuko miwili yenye nguo na begi moja.
Polisi waliuchukua mwili na kuupeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili. Hata hivyo, ndugu wa marehemu walipatikana na mwili kufanyiwa uchunguzi na daktari kisha kuuchukua na kuusafirisha kwenda Mwanza kwa mazishi.
>>>UWAZI
Social Plugin