Darasa Huru!! HAYA NDIYO MAMBO 10 YA WAKATI HUU AMBAYO BAADAYE UTAYAJUTIA



1. Kuishi maisha ambayo huyapendi au huyamudu kutoka moyoni mwako lakini kwa sababu tu unataka kuwafurahisha wale wanaokuzunguka. Unapotumia muda mwingi kutazama wale wanaokuzunguka wanakuonaje na kukuchukuliaje wewe na maisha unayoishi mwisho wake utashindwa kutambua wewe ni nani, uwezo wako na namna gani hasa unapaswa kuishi maisha yako. 

2. Kumuacha mtu mwingine akutengenezee ndoto za maisha yako. Mojawapo ya changamoto kubwa kwenye maisha ni kutambua wewe ni nani, uwezo wako na mapungufu yako na kuridhika na kile ulichokitambua. Sehemu muhimu ya kujitambua ni kutopoteza mwelekeo katika kufuata malengo na ndoto zako licha ya vikwazo unavyokutana navyo.

3. Kuwa na marafiki na watu wanaokuzunguka wenye mitazamo hasi kuhusu mambo mengi yanayohusu maisha. Mitazamo hasi ni kama kukata tamaa na kila wakati unaposhindwa kutafuta kitu au mtu wa kumtupia lawama. Mitazamo ya aina hii inaambukiza. Kumbuka kwamba kuwa na marafiki wa aina hii ni uamuzi na si jukumu la lazima na jiweke huru kutoka watu wa sampuli hii. Jitahidi kuzungukwa na watu wenye mitazamo chanya na wavumilivu. 

4. Kuwa mbinafsi. Weka jina lako katika mioyo ya watu kwa mema ukitenda yale unayopenda kwenye maisha yako. Unayojitendea mwenyewe hupotea na wewe unapopotea lakini unayowatendea wengine hubaki hata wakati ambao wewe hutakuwepo tena. 

5. Kukataa au kuyaepuka mabadiliko. Kama unataka kujua ulipotoka, tazama ulipo sasa hivi na kama unataka kujua unakoelekea tazama matendo yako leo. Njia za zamani zimekufikisha ulipo leo. Jifunze kama njia hizo zinaweza pia kukutoa ulipo leo na kukupeleka unapotaka kesho (katika nyakati mpya, watu wapya na changamoto tofauti). Kama hazitakusaidia zibadilishe.

6. Kukata tamaa mambo yanapokuwa magumu. Tazama kushindwa na kushinda kama matokeo ya mchezo. Hata mambo yanapokuja tofauti na ulivyotegemea jifunze unachoweza na songa mbele. Anayejifunza kitu kila anaposhindwa na kusonga mbele mwisho wake anashinda. Kushinda vita hutokea mapema kabla ya mapigano ya mwisho. Kushinda kunaandaliwa na zile hatua za kuelekea pambano, kushinda hakuandaliwi siku ya pambano lenyewe.

7. Kujaribu kufanya kila kitu kidogo kidogo. Hatuwezi kushinda kila kitu. Chagua kila unachoweza na wekeza nguvu zako kwake. Kila binadamu liko jambo ambalo analiweza zaidi ya jingine. Tafuta lako, lifanyie kazi.

8. Kukubali maisha yenye ubora mdogo kuliko ule ambao nguvu, vipawa na uwezo ulioojaliwa vingeweza kukupatia. Kuwa jasiri kuacha yaende yale ambayo unaona si kiwango chako na kuwa na busara kusubiri huku ukiyafanyia kazi kwa bidii yale ambayo unaamini ni kiwango chako. Kuna muda inabidi uanguke chini zaidi kuliko hapo ulipo ili uweze kusimama na kukaa juu zaidi ya hapo ulipo. Kuna muda macho yako inabidi yaoshwe kwa machozi yako mwenyewe ili uone mbele vizuri zaidi. 

9. Kila siku kukaa ukiisubiria kesho. Tatizo ni kwambo siku zote tunadhani tuna muda. Ukweli ni kwamba iko siku utagundua kwamba huna tena muda wa kufanya yale ambayo ulitamani kufanya kwenye maisha. Ikifikia hiyo siku inawezekana utakuwa umeshatenda yale uliyotamani kutenda au utakuwa na orodha ya sababu za kwa nini hukufanya uliyotamani kufanya kwenye maisha yako. Muda wa kuamua ni sasa. 

10. Uvivu na kulalamika. Hakuna mtu anaidai kitu dunia. Tumeikuta hapa na yenyewe ndio inatudai kuitunza na kuiacha bora kuliko tulivyoikuta kama waliotutangulia walivyoitunza nasi tukaikuta. Usiseme iko siku, siku ni leo. Usisema fulani atafanya hivi na vile, fulani ni wewe. Chukua jukumu. 

Dondoo kiasi toka: More Great Minds

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post