Mahakama ya wilaya Geita mkoani Geita imemhukumu Paul Kakwaya(43) kwenda jela miaka sita na kulipa faini ya shilingi milioni moja baada ya kupatikana na kosa la kumchoma kisu kifuani dada yake sehemu za maziwa Koreta Kakwaya(78).
Awali leo mwendesha mashitaka wa serikli Ester Magoti ameieleza mahakama kuwa mnamo tarehe 18 mwezi wa nne mwaka huu mnamo saa sita na nusu usiku mtaa wa katoma mjini hapa mshitakiwa alienda nyumbani kwa dada yake kwa ajili ya maongezi.
Ameongeza kuwa walipokuwa sebuleni baada ya maongezi mshitakiwa alimkaba shingo na kuchomoa kisu na kuanza kumchoma sehemu za kushoto wa ziwa huku akimsukumizia upande wa ziwa la kulia kwa lengo la kumuua na baada ya tukio hilo mtuhumiwa alimvutia chumbani na yeye kubaki sebuleni akalala.
Baada ya muda kelele zilianza kusikika kwa mama aliyechomwa kisu na majirani wakaanza kuja kwa ajili ya kutoa msaada na ndipo walipofika wakamkuta mtuhumiwa akiwa amelala sebuleni huku akionekana kama amechanganyikiwa.
Mama huyo alichukuliwa na majirani akiwa na kisu alipochomwa hadi kituo cha polisi alipopewa PF3 na kuenda kumfanyia upasuaji katika hospitali ya wilaya kwa ajili ya kukitoa kisu kwani majirani walishindwa kukitoa kisu hicho.
Mara baada ya kusomewa mashitaka hayo mahakama ilimtia hatiani na kumhukumu kwenda jela miaka 6 na kulipa faini ya shilingi milioni moja ili liwe fundisho kwa wale wote wenye nia za kutaka kufanya vitendo vya namna hiyo.
Akitoa hukumu hiyo Hakimu wa mahakama ya wilaya Zabroni Kesase amezingatia ushahidi wa pande zote na kijiridhisha kuwa mtuhumiwa alikuwa na hatia mbele ya mahakama.
Na Valence Robert wa Malunde1 Blog -Geita