Binti mwenye ulemavu wa ngozi (albino) aitwaye Sarah Maleseli (27) mkazi wa kitongoji cha Magomeni kijiji cha Ryamidati wilaya ya Shinyanga vijijini mkoani Shinyanga anasumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya ngozi kwenye shingo kwa muda wa miaka miwili sasa bila ya kupata matibabu stahiki na kulazimika kutumia dawa za kienyeji ambazo hata hivyo hazijasaidia.
Hayo yamebainika juzi wakati Umoja wa chama cha akina mama (UKIMWASE) cha kata ya Mwasele mjini Shinyanga kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la (ALBINO CHILD ORGANISATION) la nchini Marekani lilipotembelea familia ya binti huyo kushuhudia afya yake ikiwa imedhoofika.
Akitoa maelezo ya binti huyo mwenye ulemavu wa ngozi kwa niaba ya familia ,mwenyekiti wa kijiji cha Ryamidati Lucas Mwandu alisema Sarah amekuwa akisumbuliwa na kansa ya ngozi ndani ya miaka miwili sasa bila ya kupata matibabu kutokana na familia yao kukosa uwezo wa kifedha kugharamia matibabu.
Mwandu alisema binti huyo ambaye ni yatima na anaishi na bibi yake kikongwe mwenye umri miaka 70 na amekuwa akipata matibabu ya dawa za kienyeji ambazo hazina msaada wowote kwake na kusababisha ugonjwa huo kuendelea kusambaa mwili mzima.
“ Sarah aliugua ugonjwa wa kansa mwaka jana,familia yake ni maskini,tulianza kumtibu kwa dawa za miti shamba lakini hatuoni mafanikio yeyote’’,alieleza Mwandu.
“Kutokana na kukua kwa ugonjwa huo tulikaa kama wanakijiji kujadili namna ya kumsaidia binti huyu tuliafikiana kulifikisha suala hili kwanza kwa katibu wa chama cha walemavu mkoani Shinyanga tupeane ushauri ili kuokoa maisha yake”,aliongeza Mwandu.
Kwa upande wake katibu wa chama cha Albino mkoani Shinyanga Razalo Manuel alisema tayari suala hilo wameshalifikisha kwa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga vijijini Mohamed Kiyungi na sasa wanasubiri utekelezaji wake na kudai kuwa amewaahidi kughalamikia matibabu ya binti huyo ,lakini kwa upande wa usafiri na malazi ni juu ya familia hiyo.
Manueli alisema kutokana na familia hiyo kutokuwa na uwezo wa kifedha ameomba wadau na mashirika binafsi ya kutetea haki za binadamu kusaidia kutoa gharama hizo za usafiri na malazi pindi atakapokuwa anapata tiba.
Naye mwenyekiti wa umoja wa akina mama hao (UKIMWASE) Maltina Makwaiya alitumia fursa hiyo kuitaka jamii mkoani Shinyanga pamoja na wadau wa maendeleo kujitokeza kumsaidia binti huyo kwa kumpatia msaada wa matibabu ambapo anatakiwa kwenda kutibiwa katika hospital ya KCMC ya mkoani Moshi.
Umoja wa chama cha akina mama (UKIMWASE) cha kata ya Mwasele mjini Shinyanga kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la (ALBINO CHILD ORGANISATION) la nchini Marekani walitoa zawadi ya cherehani ambayo itamsaidia binti huyo kujikwamua kiuchumi.
Katika hatua nyingine waliahidi kuwajengea nyumba ya kisasa ambayo itakuwa salama katika kulinda maisha yao huku wakiomba jamii kushirikiana nao kuisaidia familia hiyo.
Na Kadama Malunde wa Malunde1 Blog-Shinyanga
Social Plugin