BAADHI ya wakazi wa jijini Tanga, wameomba uongozi wa Wilaya ya Tanga kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kuweka mkakati endelevu, utakaodhibiti wimbi la vijana wa kike wanaojiuza miili yao nyakati za usiku kwenye baadhi ya barabara za katikati ya mji na bustani za kupumzikia.
Wamesema hatua hiyo, itasaidia kukomesha vitendo hivyo vinavyoendelezwa bila woga na kudhibiti kasi ya ongezeko lao, hasa katika barabara ya Independence na Bustani ya Forodhani nyakati za jioni.
Aisha Zahoro, mkazi wa Chumbageni alisema hali ni mbaya zaidi katika Bustani ya Forodhani, ambapo wasichana wadogo hasa wale wenye umri wa kusoma shule za sekondari, wamefikia hatua ya kuvua nguo zao ili kuonesha wazi maumbile yao kwa baadhi ya wanaume, wanaofika eneo hilo kwa lengo la kuwachukua.
“Sikuamini macho yangu usiku wa saa 2 hivi, nikiwa hapo bustanini nimeketi kwenye viti vilivyoko karibu na miembe mikubwa, pembeni walisimama wasichana kadhaa nikadhani nao wamekuja kupunga upepo au kupata vyakula hapo.
Lakini kumbe sivyo, wenzangu hao walikuwa kazini…nilishangaa kwani walipofika wanaume wawili, wenzangu walianza kuzungumza nao biashara, ghafla mmoja kati yao akafunua nguo alizokuwa amevaa, akitamba kwamba ‘nitazame mimi sina kovu hata moja mwilini,” alisema.
Alisema wasichana hao wanajiuza kwa bei za kati ya Sh 2,000 kwa huduma ya haraka (chapchap) hapo hapo bustanini, Sh 5,000 kinyume na maumbile na Sh 10,000 ndani ya gari la mteja.
Alidai kwamba vitendo hivyo, sasa vimevuta wasichana wengi wadogo, ambao walipaswa kuzingatia masomo.
Hassan Sadoki alisema ili kusaidia kudhibiti hali hiyo, ambayo sasa inaleta sifa mbaya ndani ya Jiji ni vema ufanywe msako endelevu wa kuwakamata na kuwaadhibu ili iwe mfano kwa wengine, wanaotaka kuendeleza vitendo hivyo, kwa lengo la kujipatia fedha ya kujikimu kimaisha.
Kwa upande wake, Audax Msofe, mkazi wa Namiani, alisema binafsi anaamini vijana wanaofanya biashara ya ngono katika mitaa mbalimbali ya jijini humo, ikiwemo kwenye bustani, wanahitaji kujengwa kwa maadili ya kidini ili wawe na hofu ya Mungu.
“Naamini msako wa polisi peke yake hautatosha kuwadhibiti, badala yake viongozi wa dini nao washirikishwe katika suala hili kwa kuendelea kuzungumza na waumini wao hasa vijana, ambao hivi sasa wanaonekana hawana kabisa hofu ya Mungu mioyoni mwao na hivyo kuamua kujiingiza kwenye vitendo viovu”, alisema.
Social Plugin