Chakula anachokula mtu lazima kiwe na muda wa matumizi. Kutokuwa na tarehe ya ukomo wa kutumika ni kukiuka haki ya mlaji. Kama hiyo haitoshi ni lazima kiandaliwe katika mazingira mazuri na kukidhi viwango vya matumizi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Ikumbukwe kwamba asilimia 60 ya Watanzania hasa waishio mijini wamekuwa wakitumia mkate kama kifungua kinywa, hata hivyo chakula hiki kimekuwa kikitengenezwa na watu wengi bila kufuata sheria, lakini vyombo vya sheria vimekaa kimya.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti la mwananchi, umebaini kuwa licha ya uwepo wa matanuru ya kuoka mikate sehemu tofauti za nchi, wafanyabiashara wengi hasa jijini Dar es Salaam wamekuwa wakizalisha bidhaa hiyo uchochoroni na kwenye makazi ya watu, kisha kusambaza katika maduka bila kuthibitishwa ubora wake na taasisi husika za Serikali.
Maduka yakiwamo yale makubwa (supermarkets), baadhi yake yamekuwa yakitengeneza mikate inayolalamikiwa kuwa mibovu. Baadhi yake hulalamikiwa kuwa haina ubora, mingine huwa na ukungu na mingine kuwa migumu kutokana na kukaa kwa muda mrefu dukani.
Mfanyabiashara mmoja anayezalisha mikate na kuisambaza katika mitaa mbalimbali maeneo ya Tabata jijini Dar es Salaam anasema tatizo ni Serikali akidai imeshindwa kuwaongoza.
“Nilikuwa na wazo la kuanzisha kiwanda cha kawaida kwa kutumia jiko la mkaa kwa ajili ya kutengeneza mikate na kuuza katika eneo ninaloishi. Jiko langu nilinunua kwa Sh350,000, pia ukijumlisha na vifaa vingine ambavyo nilivinunua sambamba na jiko hili ni Sh450,000, nilifanya hivi kwani sikuwa na kazi ya kufanya. Nikaona nijiajiri,” alisema mfanyabishara huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Kuhusu bidhaa zake kukaguliwa na kupitishwa na Shirika la Viwango (TBS), pamoja na kibali cha Mamlaka ya Chakula na Lishe (TFDA), mfanyabiashara huyo anasema: “Sina kibali kwa kuwa niliona utakuwa mzunguko mrefu. Pili sikuwa na kiwanda maalumu, nisingefanya biashara,” anasema mama huyo anayeuza mikate yake kwa gharama ya Sh800 kwa mkate mmoja.
Kwa mujibu wa taarifa za TBS ya wiki iliyopita ni kwamba asilimia 96 ya mikate inayouzwa nchini haijathibitishwa ubora wake.
Baadhi ya wananchi wanahofia utendaji wa taasisi za TBS na TFDA kama kweli zinafaa kuendelea kuwepo ikiwa zinashindwa kudhibiti biashara hiyo, kiasi cha kuachia zaidi ya asilimia 96 ya mikate kuuzwa bila kuthibitishwa ubora wake.
Muda wa kuharibika
Hili limekuwa tatizo kubwa, mara nyingi katika maduka haya wauzaji huwabambika mikate iliyoharibika watoto na wasaidizi wa ndani.
Adamu Shayo mkazi wa jijini Dar es Salaam anahoji: “Kwanini mikate haina muhuri unaoonyesha muda uliotengenezwa, pamoja na muda wa kuharibika? Binafsi nimeshanunua sana mikate kwenye maduka makubwa (supermarkets), baadhi yake hadi huwa imeota ukungu, ila kwa sababu ya haraka unajikuta umechukua kitu kibovu,” anasema.
Shayo anasema alishawahi kurudisha bidhaa ya aina hiyo katika duka mojawapo jijini na kuambiwa na muuzaji kwamba hakuona wakati anamkabidhi iwapo mkate huo ulikuwa umeshaharibika. “Ukirudisha ndiyo mwenye duka naye anajifanya kushangaa kuwa hakuona pia. Naona ifikie hatua sasa mikate nayo iwe na tarehe ya kutengenezwa na ile ya kuharibika kama ilivyo kwa bidhaa nyingine, la sivyo tutakuwa tunalishana sumu”.
Shayo anaiomba Serikali kuboresha sheria ya chakula na kuongezewa makali, ili kuweza kuwabana wale wote wanaokwenda kinyume na sheria hiyo ili kunusuru afya za walaji na kuondoa kabisa bidhaa zisizokidhi vigezo.
Sheria ya Chakula inasema nini kuhusu suala hili
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ilianzishwa chini ya kifungu 4 (1) cha sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Na. 1 ya mwaka 2003 na iliundwa baada ya Bunge kufuta sheria ya Dawa na Sumu na sheria ya Kudhibiti Ubora wa Vyakula zote za mwaka 1978.
Moja ya majukumu ya TFDA ni kukagua viwanda vya utengenezaji na maeneo ya kuuzia bidhaa zinazodhibitiwa na mamlaka ili kuhahikisha kuwa viwango vilivyowekwa, vinafikiwa.
Kauli ya TBS na TFDA
Ofisa uhusiano wa Shirika la Viwango (TBS), Rhoida Andusamile anasema ni jukumu la wakazi wa karibu na viwanda hivyo bubu kutoa taarifa kwa shirika hilo ili kulinda usalama wa afya zao, akieleza kuwa bidhaa zote zina sheria iliyowekwa kabla ya kutengenezwa na kisha kumfikia mlaji.
“Ubora wa bidhaa yoyote ile una utaratibu wake, mtu haruhusiwi kutengeneza bidhaa hasa vyakula kama mikate na vinginevyo bila kuwa na kibali kutoka TBS na pia awe amesajili bidhaa yake hiyo TFDA ambao na wao watajiridhisha kuhusu bidhaa yake kama inafaa kupelekwa kwa walaji au la,” anasema Rhoida.
Anasema wamekuwa wakilazimika kutoa elimu kwa umma, akitoa mfano wa kipindi cha mwezi Agosti hadi Desemba mwaka jana walipotoa elimu na kukamata waliokaidi agizo la kuzalisha mikate kwa kufuata sheria.
Anasema mikate yoyote inayotengenezwa, ni lazima ifikie kiwango ambacho kitakuwa kimekubaliwa na Tbs.
“Iwapo tutagundua uwapo wa bidhaa zisizo na ubora, tutachukua jukumu la kuondoa bidhaa hizo sokoni, kufuta leseni ya mhusika, kuweka utaratibu wa marejesho au fidia, kuweka taratibu za kuharibu bidhaa duni au kuzirudisha zilikoagizwa na kutoza faini.
“Sheria hii imeambatana na kanuni nne za utekelezaji ambazo ni kanuni za usimamizi wa alama ya ubora, ithibati ya ubora, upimaji wa bidhaa, ithibati ya ubora wa shehena na kanuni za usalama wa chakula,” alisema Rhoida.
Ofisa uhusiano wa Mamalaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia Simwanza anasema mara nyingi inakuwa vigumu kudhibiti mikate hasa kwa wale wanaotengeneza kiholela mitaani.
“Februari mwaka huu kuna maduka ya kuoka mikate tuliyafungia. Hiyo ilitokana na wao kutokidhi vigezo vile vilivyowekwa. Wapo ambao hawakuwa wamesajili na wengine tulibaini kwamba wameanza kutengeneza mikate isiyokidhi viwango. Wapo tuliowapa muda wa kurekebisha hilo na wengine tuliwafungia kwa miezi mitatu ili wajirekebishe na kutimiza maagizo tuliyowapa,” anasema Simwanza.
Na Herieth Makwetta, Mwananchi