Mahakama ya mwanzo ya Old Shinyanga mkoani
Shinyanga imemhukumu mwanamke mmoja Pendo
Joachim (33) mkazi wa kata ya Old Shinyanga kutumikia kifungo cha nje ya
gereza kwa muda wa miezi 12 na kulipa faini ya shilingi milioni moja baada ya
kupatikana na kosa la kusingizia mtoto kwa mwanaume mwingine ili apate pesa za
matumizi.
Akitoa hukumu hiyo jana,hakimu wa mahakama
ya mwanzo ya Old Shinyanga Christina Chovenye alisema mahakama hiyo baada ya
kuridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi imemhukumu Pendo Joachim
kutumikia kifungo cha nje cha miezi 12 na faini ya shilingi milioni moja ili
liwe fundisho kwa watu wengine.
Chovenye alisema mahakama hiyo imemtia
hatiani Pendo Joachim chini ya kifungu cha sheria cha 304 sura ya 16
kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kwa kosa la udanganyifu ambapo Deus Njile
amekuwa akimuhudumia mtoto huyo kwa muda wa miaka 3 akijua kuwa ni mtoto wake
Kwa upande wake mshitakiwa Pendo Joachim
alipotakiwaa kujitetea aliomba kupunguziwa adhabu kwa kuwa ana watoto wawili
wanaomtegemea na kwamba anasumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu.
Deus Njile alisema
kuwa alibaini kuwa mtoto sio wake baada ya kuona kadi mbili za kliniki zenye
majina tofauti ya baba ndipo alipoamua kwenda kwenye uongozi wa kijiji ili
kupata suluhu ndipo Pendo Joachim alikiri kuwa mtoto huyo ni wa mwanaume
mwingine.
Katika Kesi hiyo yenye namba 24 ya mwaka 2014 ili
funguliwa tarehe 19/3/2014,imeelezwa kuwa Pendo Joachim alikuwa
akisingizia kuwa mtoto wake anayetumia jina la Edward Deus ni wa bwana Deus
Njile na kusababisha Deus Njile kumhudumia mtoto huyo kama wa kwake kwa muda wa
miaka mitatu.