Wakitumia utafiti wa moja kwa moja wa kuwahusisha wanywa pombe 2,042 kwa kuangalia mienendo yao wakati wametumia pombe au kutokutumia, walibaini kuwa kuna tofauti kubwa ya kimwili.
“Imebainika kuwa kunywa glasi tatu kubwa za mvinyo kunaweza kuusukuma mwili kwenye kilele ambacho ni cha kutumia zaidi chakula ndani ya saa 24, ambacho kitampatia nguvu ya ziada,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Nguvu inayoongezeka kwa kiwango hicho cha pombe imebainika kuwa na 6,300 za ziada tofauti na asingekunywa.
Ikaonekana kuwa pombe huchochea pia mtu kula vyakula vyenye protini kwa wingi hususan nyama.
Pamoja na faida hiyo, ugunduzi huo umebaini kuwa, watu wanaokunywa pombe wanajiingiza kwenye mazingira mabaya ya kuongeza uzito kupita kiasi.
Kutokana na kula huko kulikopitiliza, ugunduzi huo umebaini wanywa pombe wasipojitahidi kufanya mazoezi wanajiweka katika hatari ya kupata maradhi kama vile ya kisukari na moyo.
Mtaalamu wa Lishe aliyesimamia utafiti huo, Dk Jacquie Lavin anasema kinachoonekana ni kwamba aliyekunywa pombe hopoteza ule uwezo binafsi wa kujisimamia juu ya kiwango cha chakula anachopaswa kukitumia.
Anasema wanaokunywa pombe wana kawaida ya kuongeza uwezo wa kula na wanaweza kudumu mezani kwa muda mrefu wakila, hasa inapokuwa chakula ni kizuri na chenye lishe nyingi.
“Pombe hufanya chakula kionekane bado kinahitajika mwilini. Huwa inaamsha hisia za kuona chakula ni kitamu kuliko vile angekihisi katika hali ya kawaida akiwa hajanywa pombe,” anasema Dk Lavin.
Mtaalamu huyo wa Taasisi ya Slimming World aliishauri Serikali ya Uingereza iamuru kampuni za vileo ziongeze maelezo ya ziada kwenye lebo zake.
Miongoni mwa maelezo aliyopendekeza ni vileo vyote kuwa na maelezo kwamba vinachochea uwezo wa kula kwa kuwa huo ndiyo ukweli kwa watumiaji.
Utafiti wapondwa
Wanasayansi kadhaa waliopitia utafiti huo waliupongeza lakini wakasema una udhaifu wa maelezo ya kisayansi.
“Utafiti huu unavutia sana lakini umejikita zaidi kwenye kuchunguza mienendo ya tabia za wanywa pombe. Haujachambua mwili kisayansi namna pombe inavyochochea kula,” anasema mtaalamu wa Taasisi ya Lishe ya Uingereza (BNF), Bridget Benelam.
Hata hivyo, anausifu utafiti huo kwa kuwa unamweka wazi mtu kufahamu hali halisi inayoweza kumpata anapotumia pombe.
Mkuu wa Taasisi ya Afya ya Jamii nchini Uingereza (PHE), Dk Alison Tedstone alisema uchunguzi huo umeiweka jamii kufahamu nguvu ya ziada inayotokana na matumizi ya pombe.
“Kalori za ziada anazopata mtu kwa kula chakula zinaweza kumsababishia kuongeza uzito wa ziada utakaomweka katika hatari ya kupata maradhi ya moyo, kisukari na baadhi ya saratani,” alisema Dk Tedstone.
Ingawa utafiti huo ni wa karibuni, Dk Tedstone anajigamba kuwa taasisi yake tayari imekuwa ikiwasisitizia watu kanuni za kuishi muda mrefu kwa usalama kwa kula vizuri, kufanya mazoezi na kuwa waangalifu kwa kuwa wa kiasi katika matumizi ya pombe na chakula.
Waziri Kivuli wa Afya nchini Uingereza, Luciana Berger alisema utafiti unaonyesha wazi kuwa ipo haja ya kuielimisha jamii kuhusu uhusiano wa pombe na uzito.
Alionya kuwa jamii inapaswa kuwa makini kwa sababu Serikali hutumia kila mwaka Paundi 5 bilioni sawa na Sh13.8 trilioni, kuhudumia watu wenye uzito uliopitiliza.
Mtaalamu wa Lishe anayeendesha shughuli binafsi jijini Dar es Salaam, Deodatus Minja anasema utafiti huo umejikita zaidi kwa watu wa Ulaya ambako hakuna tatizo la chakula.
Anasema ulipaswa kuangalia pia nini kinatokea iwapo mtu atakunywa pombe na akapata hamu ya kula lakini akakosa au akatumia kwa kiwango kidogo.
Anasema katika nchi maskini, baadhi ya wanywa pombe wanakuwa wadhoofu kiafya jambo linaloashiria kuwa wanaathirika.
“Pengine uchunguzi huo ungeingia kwa undani zaidi ungeweza kubaini kuna madhara ya matumizi ya pombe katika lishe kidogo,” anasema Minja.
Anasema kwa kuiangalia tu jamii, athari za afya dhaifu huwapata zaidi wanaokunywa pombe katika umaskini wa kipato.
“Ukiangalia wale wenye fadha za kunywa na kula vizuri ndio hao wanakuwa na ama afya nzuri au uzito kupita kiasi. Hii inadhihirika wazi kulingana na utafiti huo,” anasema Minja.
Imeandikwa na Leon Bahati kwa msaada wa mitandao