Historia yawekwa Shinyanga!! MAANDAMANO MAKUBWA KULAANI KUNDI LA BOKO HARAM HUKO NIGERIA KUTEKA WASICHANA YAFANYIKA,ASMK FOUNDATION SHINYANGA YAONGOZA MPANGO MZIMA,TUKIO ZIMA LIKO HAPA


Leo mkoa wa Shinyanga nchini Tanzania umeweka historia kubwa hapa  dunia baada ya kuungana na jumuiya ya kimataifa kwa kufanya maandamano ya amani yaliyoandaliwa na taasisi ya ASMK Foundation ya mjini Shinyanga inayojihusisha na msisitizo wa elimu kwa wanawake lengo likiwa ni kulaani matukio ya kundi la Boko Haram kuteka wasichana zaidi ya 200 huko Nigeria na kuwapeleka kusikojulikana.

Pichani ni baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebeba ujumbe wa kila aina.

Hapa ni kwenye ofisi za taasisi  isiyokuwa ya kiserikali  ya ASMK Foundation ambayo ipo nyuma ya jengo NSSF mjini Shinyanga mkabala na barabara ya Nyerere.

Leo wananchi wa mkoa wa Shinyanga nchini Tanzania wameungana na jumuiya ya kimataifa kwa kufanya maandamano mjini Shinyanga lengo likiwa ni kukemea maovu waliyofanyiwa wasichana zaidi ya 200 katika jimbo la  Borno nchini Nigeria ambao hivi karibuni wakiwa shuleni walitekwa na kundi la Boko haram na kupelekwa msituni kwa madai kuwa hawapaswi kusoma bali ni wa kuolewa tu.

Maandamano yalianzia kwenye ofisi za ASMK Foundation na kupitia katika maeneo mbalimbali kama vile barabara ya Nguzo nane,soko la Nguzo nane,Zimamoto,Bakurutu,Mnara wa Voda,Uhuru Sekondari,soko kuu  na baadaye kuishia katika viwanja vya Mazingira senta mjini Shinyanga huku mgeni rasmi akiwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga ndugu Annarose Nyamubi.

Wa pili kulia ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga ndugu Annarose Nyamubi wakati wa maandamano yaliyoandaliwa na ASMK Foundation ya mjini Shinyanga ambao wameguswa na kusikitishwa na matukio ya hivi karibuni huko Nigeria ambapo wasichana zaidi ya mia mbili wametekwa na kundi la Boko Haram kwa madai kuwa watoto wa kike wanatakiwa kuolewa tu badala ya kusoma.ASMK pia wameshirikiana na umoja wa vijana wa Umoja wa Mataifa Shinyanga(UNA) kufanikisha maandamano hayo

Wa kwanza kulia ni Theresia Makwaia mjumbe kutoka ASMK Foundation akiwa ameshikilia bango linalosomeka "Elimu kwa wanawake ni ukombozi kwa jamii",wa pili kushoto kwake ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga ndugu Annarose Nyamubi akiwa ameshikilia bango wakati wa maandamano kulaani na kukemea maovu yanayofanywa na Boko Haram huko Nigeria na kuomba kwa dua wasichana waliotekwa waachiwe huru pasipo madhara

"Bring Back Our Girls" ikiwa na maana ya "Turejeshee ama turudishie wasichana wetu" ni miongoni mwa mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji mjini Shinyanga wakiwemo ,watoto,wanafunzi,shule za msingi,sekondari wa vyuo,akina mama n.k 

Kushoto ni mwenyekiti wa umoja wa vijana wa umoja wa mataifa Shinyanga(UNA-Tanzania) Ezra Manjerenga akiwa na Pafra mwenyekiti wa YUNA chapter chuo cha VETA mjini Shinyanga nchini Tanzania wakiwa wameshikilia bango wakati wa maandamano leo.UNA-Tanzania wameshirikiana na ASMK kufanikisha maandamano ya amani ya kulaani kitendo cha kundi la Boko Haram kuteka wasichana zaidi ya 200 na kuwapeleka msituni
Waandishi wa habari nao walikuwepo katikati ni bwana Thomas Masanja mwandishi wa habari radio Sibuka fm,wa kwanza kulia ni bwana Kadama Malunde mkurugenzi wa  Malunde1 Blog

Watoto nao hawakuwa nyuma katika maandamano hayo ambayo yamefanyika wakati wa wiki ya elimu hapa nchini,ambapo taasisi hiyo inalipa kipaumbele suala la watoto kupelekwa shule ikiwa ni haki yao ya msingi.

Wa kwanza kulia Steve Kanyefu mwandishi wa habari radio Faraja fm,wa tatu kutoka kulia ni mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo ya ASMK Foundation bi Liliane Sykes Kwofie akiwa ameshikilia bango linalosomeka "Real Men Do Not Buy Girls" ambaye alisema ASMK Foundation inalaani maovu yote dhidi ya akina mama wakongwe popote ulimwenguni pamoja na kupinga vitendo vya unyanyasaji,ubakaji,ukeketaji sambamba na kupigwa na kunyimwa haki ya elimu kwa watoto wa kike. wakati wa maandamano hayo leo mjini Shinyanga  nchini Tanzania

Usalama kwa waandamanaji ulikuwa wa kutosha kwa waandamanaji,kama unavyoona pichani ni askari wa usalama barabarani akifanya yake katika barabara ya Bakurutu mjini Shinyanga wakati wa maandamano ya kulaani vitendo vya Boko Haram nchini Nigeria ambapo leo mkoa wa Shinyanga umetengeneza historia kubwa duniani kwa kujiunga na jumuiya ya kimataifa kuwaombea duna wasichana waliotekwa na kundi la Boko haramu waachiwe huru kwani sasa hivi wako mikononi mwa kundi hilo hatari

Waendesha baiskeli maarufu kwa jina daladala mjini Shinyanga nchini Tanzania pia hawakuwa nyuma kulaani vitendo vya kundi la Boko Haram ambalo linajihusisha na mauaji ya holela,ubakaji na uhalifu wa mali nchini Nigeria.Kama unavyoona mabango katika baiskeli zao

Mbele wa kwanza kushoto ni mfanyakazi wa kujitolea katika taasisi ya ASMK Foundation bwana Joseph Makwaia,kulia kwake ni Dkt Sam Kofwie mkurugenzi wa ASMK Foundation  Shinyanga wakiwa katika maandamano yaliyolenga kulaani vitendo viovu dhidi ya akina mama wakongwe popote ulimwenguni pamoja na kupinga vitendo vya unyanyasaji,ubakaji,ukeketaji sambamba na kupigwa na kunyimwa haki ya elimu kwa watoto wa kike.


Maandamano yanaendelea,mbele kushoto ni mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo ya ASMK Foundation bi Liliane Sykes Kwofie akiwa ameshikilia bango linalosomeka "ASMK Foundation Shinyanga,Ukatili kwa mtoto wa kike sio sawa","Bring Back Our Girls"

Ni katika viwanja vya Mazingira senta ambako maandamano hayo yalipoishia,ambapo mkuu wa wilaya ya Shinyanga Anna rose Nyamubi alikuwa mgeni rasmi,huku watu mbalimbali wapenda maendeleo wakiwemo viongozi wa dini wakihudhuria kwenye hafla ya mapokezi hayo ya maandamano hayo ya amani kupinga vitendo viovu kote duniani

Watoto wenye ulemavu wa ngozi,wasiosikia na wasioona wanaoishi katika kituo cha Buhangija jumuishi katika manispaa ya Shinyanga nchini Tanzania wakiimba wimbo wakati wa hafla ya mapokezi ya maandamano,wimbo ulikuwa na ujumbe mzito...nanukuu baadhi ya maneno "Watoto wapelekwe shule,dunia imeharibika binadamu wao kwa wao wanauana,Albino tunauawa,albino tunaishi kwa mashaka hatujui hatma ya maisha yetu,albino tunaishi kwa tabu na mateso..."

Aliyesimama ni mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo ya ASMK Foundation bi Liliane Sykes Kwofie akizungumza wakati wa hafla ya mapokezi ya maandamano ambapo alisema taasisi yake inayohusika na maendeleo ya jamii inalaani maovu yanayofanywa na Boko Haram nchini Nigeria na mengine yote yanayofanyika kote duniani huku akiwataka wananchi wa mkoa wa Shinyanga nchini Tanzania kusimama kidete katika kupiga vita mauaji ya vikongwe pamoja na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ambapo hivi karibuni kumezuka wimbi la watoto kubakwa,kulawitiwa na kutobolewa macho.

Aliyesimama ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga Annarose Nyamubi akitoa hotuba yake katika viwanja vya Mazingira mjini Shinyanga nchini Tanzania ambapo alisema maandamano hayo yamefanyika wakati wa wiki ya elimu hivyo kuitaka jamii kupeleka watoto wa kike shule badala ya watoto kuolewa.Mbali na kulaani kundi la Boko haram kuteka wasichana pia alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa mkoa wa Shinyanga pamoja na viongozi wa serikali ,siasa, dini  na vyombo vya ulinzi na usalama kushirikiana kwa pamoja kupinga ukatili unaofanywa mkoani Shinyanga nchini Tanzania dhidi ya watoto wa kike wanaobakwa na kutobolewa macho na mauaji ya vikongwe.Aliyekaa kulia ni Askofu Charles Ngusa wa kanisa la Anglican dayosisi ya Shinyanga,kushoto aliyekaa ni Mchungaji Jack Grubbs kutoka Potomac Falls Anglican church ,Virginia nchini Marekani

Aliyesimama ni Imamu mkuu wa Masjid Ibadhi Shinyanga Mrisho Maulid ambaye pamoja na mambo mengine alisema miongoni mwa sababu zinazopekea kuongezeka kwa maovu katika jamii ni pamoja na watu kukosa elimu ya kumwamini mungu huku wengine wakitawaliwa na imani za kishirikiana kwa kuamini kuwa wanaweza kupata utajiri.

Shughuli nzima ilimalizika kwa maombi kuwaombea wasichana waliotekwa na kundi la Boko haram nchini Nigeria ili wachiwe huru pasipo na madhara .

Picha zote na Kadama Malunde wa malunde1 blog


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post