Kufuatia serikali kuipandisha hadhi hospitali ya mkoa wa Shinyanga na kuwa hospitali ya rufaa na kupandishwa kwa gharama za matibabu imeelezwa kuwa hali hiyo itasababisha akina mama wajawazito wenye kipato cha chini kurudi kujifungulia kwa waganga wa jadi.
Hayo yamesemwa juzi na afisa mtendaji wa kata ya Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga James Dogani kwenye kikao cha kuhamasisha akina baba kwenda kliniki na wake zao ambapo alisema akina mama wajawazito wataanza kukimbilia kwa waganga wa jadi na wakunga wa jadi wasiokuwa na vifaa vya kitaalamu kutoa huduma ya uzazi.
Afisa mtendaji huyo alisema sera ya serikali kuzipandisha hospitali za mkoa hapa nchini na kuwa za rufaa kuharakisha bila ya kuangalia hali ya jamii inayozunguka hospitali hizo.
Dogani alisema hospitali ya mkoa wa shinyanga ilikuwa tegemeo la wananchi walio wengi hasa wenye kipato duni lakini kupandishwa hadhi na kuwa ya rufaa na kupandishwa gharama za matibabu kunaumiza wananchi.
“Asilimia wanategemea hospitali hii,wengi wanatoka vijijini na wana kipato duni lakini kuongezeka kwa gharama hizo kutasababisha wananchi kurudi kupata huduma kwa waganga wa kienyeji” alisema Dogani.
“Katika kata yangu ya Ndembezi nimeshapokea malalamiko mengi kutoka kwa akina mama wajawazito pamoja na kesi za kutelekezwa kwa ujauzito wao ,na mafarakano ya ndoa, kuwa waumezao wamekuwa wakiwafokea kwanini ameshika ujauzito bila makubaliano na wakati gharama za uzazi zimepanda ambapo mtoto wa kiume kujifungua shilingi elfu 80,kike 70, oparesheni laki tatu tofauti na hapo awali ilikuwa bure”,aliongeza Dogani.
Naye diwani wa kata ya Kitangili George Kitalama alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi mkoani humo kujiunga na mifuko ya bima ya afya ambayo itawasaidia kuwapunguzia gharama za matibabu.
Diwani huyo pia alizitaka pia halmashauri kukamilisha miradi ya vituo vya afya na zahanati kwa kila kijiji kata hali ambayo itasaidia katika kuondoa changamoto za kuongezaka kwa vifo vya mama na mtoto.
Kwa upande wake mratibu wa afya ya uzazi na mtoto katika manispaa ya Shinyanga Magreth Mzirai anayefanya kampeni ya kuhamasisha watendaji wa vijiji, kata na viongozi wa kitongoji kutoa elimu kwa akina baba kuwa wanahudhuria kliniki na wake zao ili pale unapotolewa ushauri nasaha na watalaamu wazingatie wote ikiwa ni pamoja na kupata ushauri wa uzazi wa mpango.
“Akina baba wanapokuwa wanahudhuria kliniki na wake zao itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kuzaa hovyo pamoja na kuondoa maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ,faida nyingine ni kupata taarifa za mke wako na mtoto wako afya zao zinaendeleaje hali ambayo itasaidia kupata mtoto aliye salama na mwenye afya”,alieleza Mzirai