Ikiwa ni mwezi mmoja tangu mlinzi wa kampuni ya K.K.security mjini Geita kuchinjwa hadi kufa na mwili wake kutupwa kwenye mgahawa chini ya meza katika eneo la Mbugani katika Kata ya Kalangalala mkoani hapa, mlinzi mwingine ameuawa kwa kuchinjwa usiku wa kuamkia leo mjini hapa.
Tukio hilo limetokea usiku wa wa kuamkia leo katika mtaa wa Shilabela ambapo mlinzi huyo aliyejulikana kwa jina la Juma Sunguta(48) anayeishi mtaa wa Moringe amechinjwa na kuuawa wakati akiwa katika eneo lake la kazi analolinda lililoko shilabela .
Imeelezwa kuwa mlinzi huyo ameuawa lakini wauaji hao hawakuchukua kitu chochote zaidi ya kumchinja na kuondoka.
Baadhi ya watu wa eneo hilo waliioongea na mwandishi wa habari hizi baada ya kufika kwenye eneo la tukio wamedai kuwa huenda ni chuki za kulipizana visasi kwa sababu hapo kazini alikuwa anafanya kazi vizuri.
Afisa mtendaji wa kata ya Kalangalala Hussen Hamadi aliyefika kwenye eneo la tukio amesema kuwa yeye amepigiwa simu asubuhi kuwepo kwa tukio hili na alipoenda akakuta marehemu ametupwa nje ya maduka huku shingo ikiwa imechinjwa .
Aidha Hamad ameongeza kuwa hali hiyo inasikitisha katika kata yake kwani hivi karibuni mlinzi mwingine naye aliuawa eneo la mbugani kwa hiyo kuna kila sababu ya kutafuta chanzo cha matukio hayo.
Baadhi ya wakazi waliokuwa katika eneo hilo ambapo ni eneo la maduka alipokuwa analinda marehemu wameiomba serikali kutafuta ufumbuzi wa matukio ya mauaji yamekuwa mengi na hivyo kuishi kwa wasiwasi.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa kamishina msaidizi Joseph Konyo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini waliofanya unyama huo na kisha wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Na Valence Robert Geita.
Social Plugin