JAMAA ANAYEZUNGUKA DUNIA KWA KUTEMBEA KWA MIGUU AWASILI NCHINI

Raia wa Urusi, Sergey Chikachev anayetembelea mataifa mbalimbali kwa miguu, tayari amekwisha tembelea mataifa 80 na hivi sasa yupo nchini. 
Picha na Dionis Nyato

Moshi. Raia wa Urusi, Sergey Chikachev anayezunguka mataifa mbalimbali duniani kwa miguu, juzi amewasili nchini akitokea Kenya na anatazamiwa kuzunguka mikoa mbalimbali kwa siku 30.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi jana, Chikachev ambaye ameshazunguka mataifa 80, alisema akiwa nchini, atakwenda vijijini kujifunza utamaduni na maisha ya makabila mbalimbali.

“Kwa siku chache tangu niwasili hapa (Moshi) nimebaini Watanzania ni watu wenye hazina kubwa ya ukaribu… naamini nitajifunza mengi yatakayonisaidia kuandika kitabu changu,”alisema.

Chikachev alisema atakitumia kitabu chake hicho, kupeleka ujumbe wa amani kwa mataifa hayo na kuhamasisha urafiki kati ya makabila ya mataifa mbalimbali atakayoyatembelea duniani.

Kwa mujibu wa Chikachev, alianza kutembelea mataifa hayo kwa miguu tangu mwaka 2004 na ameshazunguka Ulaya, Asia, Australia, Marekani na sasa bara la Afrika ambapo kwa sasa yupo nchini Tanzania.

Chikachev alisema baada ya kumaliza safari yake nchini, anatarajia kwenda Uganda, Rwanda, Burundi, Namibia, Botswana, Congo, Nigeria na baadaye Cameroon na atahitimisha ziara zake hizo mwaka 2017.

Hata hivyo alisema safari yake hiyo imekuwa ikikutana na changamoto nyingi na wakati mwingine amekuwa akipata lifti kutoka kwa madereva wa malori lakini hilo limekuwa likitokea mara chache.

Raia huyo wa Urusi alisema kwa baadhi ya mataifa, amekuwa akipatiwa ufadhili wa usafiri wa ndege au majini katika maeneo ambayo hawezi kutembea kwa miguu kutoka taifa moja kwenda lingine.

via>MWANANCHI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم